Breaking News

Your Ad Spot

Oct 28, 2010

ASHA-ROSE MIGIRO AKUTANA NA HILARY CLINTON; NI KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA AZIMIO LA WANAWAKE NA AMANI NA USALAMA

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro akibadilishana busara na waziri wa mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton, kabla ya maadhimisho ya miaka kumi ya Azimio namba 3525, kuhusu wanawake na Amani na Usalama. Maadhimisho hayo yaliyojikita zaidi katika majadiliano kuhusu mafanikio na changamoto za utekelezaji wa  azimio hilo tangu lilipopitishwa na baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa, mwaka 2000, yalifanyika makao makuu ya UN, Oktoba 26, 2010 mjini New York, Marekani. (Picha kwa Hisani ya UN).
======================================================================
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK

Wakati Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa likiadhimisha miaka kumi tangu kupitishwa kwa Azimio namba 3525 kuhusu nafasi na mchango wa wanawake katika masuala ya amani na usalama, vitendo vya ukatili wa kijinsia dhini ya kundi hilo la jamii bado vimeendela kushamiri hasa katika maeneo yenye vita na migogoro.

Maadhimisho ya Azimio hilo ambayo yamefanyika Octoba 26 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, kumelifanya Baraza hilo lenye wajibu wa kusimamia masuala ya amani na usalama wa kimataifa, kutoa wito tena wa kutaka kutokomezwa kwa ukatili dhidi ya wanawake pamoja na kuongeza kasi ya ushiriki wao katika mchakato mzima wa utafutaji wa amani, usalama na ujenzi wa amani hiyo.

Katika salamu zake kwa Baraza hilo wakati wa maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki Moon, ameeleza kuwa utekelezaji wa Azimio hilo, utafanikiwa pale tu ukatili wa kijinsia na udhalilishwaji wanaofanyiwa wanawake na wasichana utakapomalizwa na wahusika kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Akasema Ban Ki Moon. “ Tukio la kubakwa kwa wanawake na wasichana zaidi ya 200 lililofanywa na kundi la waasi mwezi julai mwaka huu huko mashariki ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, ni kielelezo cha wazi kabisa, kwamba bado wanawake na wasichana wanaendelea kuishi katika mazingira hatari na magumu. Hatuwezi kutekeleza kikamilifu Azimio hili kama ukatili huu hautakomeshwa nakumalizwa kabisa”.

Akabainisha kuwa mkono wa sheria ni lazima ufuate mkondo wake kwa wale wote wanaobainika kuutekeleza unyama huu, bila ya kujali kama ni sehemu ya serikali au wasio ndani ya serikali.

Akaeleza kuwa licha ya misingi madhubuti na matumaini yaliyowekwa na Azimio hilo, bado inakuwa vigumu kueleza au kutambua mafanikio ya waziwazi ya Azimio hili. Hasa ikizingatiwa kwamba inakuwa vigumu sana kusimamia haki za wanawake katika maeneo mengi yenye vita.

Jumla ya wazungumza 90 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, walizungumza katika maadhimisho hayo, ambapo mwakilishi wa Tanzania katika Umoja huo, Balozi Ombeni Sefue, alipopata nafasi ya kuzumgumza pamoja na mambo mengine alisisitiza haja na umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika utafutaji wa amani kwa kile alichosema wao ni wadau muhimu.

Aidha akasema kuwa katika kuzingatia nafasi sawa katika jamii, wanawake ni lazima wakawa na haki na fursa kamili ya uundaji wa sera zinazohusu siasa, uchumi na maendeleo ya jamii.

“Wakiwa ni wahanga wa ubaguzi, walengwa wa machafuko, kama mama na wazalishaji, wanawake wanamchango mkubwa katika uzuiaji wa machafuko, utafutaji wa amani na masuala yote yanayohusu amani na usalama” akasistiza Balozi Sefue katika Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bi Hilary Clinton.

Akaeleza kuwa katika kile kinachoitwa mila na tamaduni au hata usalama, mwanamke bado ameendelea kubaguliwa na mara nyingine kuwekwa kando wakati wanaume wanajadiliana kuhusu makubaliano ya amani.

Hata hivyo anasema Balozi Sefue “ Tanzania inapata matumaini pale ambapo wanawake wenyewe wamejitokeza kuupigia kelele mfumo huu na huku wakikazania na kudai ushiriki wao kama wadau muhimu katika jamii”

Akasisitiza kwamba mchango wao lazima utambuliwe na juhudi zaidi za kuwaunga mkono zifanyike kwa kwajengea uwezo kupitia mitandao yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uzuiaji wa machafuko.

Akasema Tanzania inaungana na wajumbe wengine wa kutaka wale wote wanaohusika na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na wasichana kufikishwa mbele ya mkono wa sheria bila ya kujali nafasi zao au nyadhifa zao.

Azimio namba 3525 lilipitishwa na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, Octoba 31 mwaka 2000. Likihitimisha mijadala mbalimbali ya miaka mingi iliyopigiwa chapuo na taasisi za kijamii na makundi ya wanawake kwa lengo la kuizidua jumuia ya kimataifa na kukomesha vitendo visivyo ya kibinadamu dhidi ya wanawake na watoto wa kike pamoja na ubaguzi wanaofanyiwa wa kutoshirikishwa katika utoaji wa maamuzi hususani katika maeneo yenye vita.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages