Breaking News

Your Ad Spot

Mar 20, 2011

JK AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUWAIMARISHA KIMAADILI NA KIROHO WAUMINI WAO HALI AMBAYO ITASAIDIA PIA USTAWI DUNIANI


Muadhama Polycarp Kadinali Pengo akimvika kofia ya kiaskofu Mhashamu Gervas John Nyaisonga  wakati wa ibada ya kumweka wakfu askofu huyo iliyofanyika mjini  Dodoma leo asubuhi.Kushoto ni  Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashmau Yuda Thadei Ruwaaichi ambaye nahammia jimbo Kuu la Mwanza(picha na Freddy Maro).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi wa dini kuongeza kasi yao katika kulilea taifa kiroho na maadili katika dunia ya sasa ambapo
maadili mema ya jamii pamoja na mila na desturi havionekani kupewa thamani kubwa.

Aidha, Rais Kikwete amewataka viongozi wa kiroho kuendelea kuwahimiza Watanzania pamoja na viongozi wa siasa kuvumiliana kwa tofauti za rangi, kabila, dini na siasa na pia kuendelea kuombea amani na utulivu wa Tanzania na upendo miongoni mwa Watanzania.

Vile vile, Rais Kikwete amethibitisha, kwa mara nyingine, azma ya Serikali yake kuendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuboresha huduma za kijamii nchini za elimu na afya kwa sababu katika hilo shabaha ya dini na Serikali haitofautiani.

Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumamosi, Machi 19, 2011, kwenye Viwanja vya Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Msalaba mjini Dodoma alipohudhuria Ibada Maalum ya kumwekea wakfu na kumsimika Askofu Mteule Gervas John Nyaisonga kuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma. (pichani)

Katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na maelfu kwa maelfu ya wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani ikiwamo ya Mbeya na Mwanza, pamoja na Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, Rais Kikwete amewaambia waamini hao:

“Napenda kutumia nafasi hii pia kuwaomba viongozi wa dini muendelee kufanya kazi ya kulilea taifa letu kiroho na kimaadili. Natambua ugumu wa kazi hiyo katika dunia ya leo ya utandawazi ambako maadili mema ya jamii pamoja na mila na desturi zetu havionekani kupewa thamani kubwa. Siku hizi mtoto mdogo kumtukana mtu mzima au watu wazima kutoleana lugha chafu, na kutositiri maungo, havionekana kuwa mambo yasiyofaa.”

Ameongeza: “Ati huo ndiyo usasa na uhuru wa kutoa maoni. Naambiwa huko kwenye mitandao ndiyo usiseme, kunahitaji moyo wa ujasiri kuhimili mambo machafu yaliyomo na lugha inayotumika. Mimi na wenzangu katika Serikali kwa kutumia vyombo vya dola tunajitahidi sana na tunaendelea na juhudi hizo. Pamoja na hayo, jamii na hasa viongozi wa kiroho mnayo nafasi maalum ya kuweza kusaidia katika mapambano hayo. Ninyi ni viongozi mnaoheshimika sana katika jamii na kauli zenu zinabeba uzito wa aina yake.”

Kuhusu ombi lake kwa viongozi wa dini kuendelea kuombea amani katika Tanzania na upendo miongoni mwa Watanzania, Rais Kikwete amesema: “ Jambo jingine ninalowaomba viongozi wa dini msichoke kufanya ni kuombea na hasa kuhubiri amani ya nchi yetu na upendo miongoni mwa wananchi wake. Jambo kubwa la kusisitiza hapa ni kuwataka watu wasibaguane kwa rangi, kabila, dini, maeneo wanayotoka ama itikadi za kisiasa. Haya ni miongoni mwa tunu ambazo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliatuachia. Ndiyo siri ya amani na utulivu wa nchi yetu.”

Amesisitiza Rais: “Msichelee kumkemea mtu yoyote anayetaka kuwagawa Watanzania kwa rangi, kabila, dini, jinsia na maeneo watokayo. Tukishindwa katika hili, amani na utulivu vitatuponyoka na hilo likitokea haitabiriki lini tutaipata tena. Na sisi tutakuwa kama walivyo wenzetu wengine ambao sote tunawajua. Hivi sasa wanahangaika kuitafuta amani na kurejesha utulivu waliokuwa nao kabla ya machafuko.”

Kwa upande wa ushirikiano katika utoaji wa huduma za jamii, Rais amesema kuwa sasa Serikali imeanza kutoa mikopo ya elimu ya chuo kikuu kwa vyuo vyote nchini bila kubagua. Kabla ya hapo mikopo ilikuwa inatolewa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Serikali tu.

Kuhusu afya, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali imekuwa inatoa ruzuku kwa hospitali na zahanati za mashirika ya dini chini ya makubaliano maalum ya kutoa huduma (service agreement).

Chini ya makubaliano hayo, ruzuku ya Serikali kwa kitanda kimoja katika hospitali za dini imeongezeka kutoka sh 7,500 kwa kitanda hadi kufikia sh 50,000 kwa sasa na kulikuwapo na vitanda 5,600 katika hospitali 60 vilivyokuwa chini ya mpango huo mwaka 2009 na sasa vimeongezeka.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages