Breaking News

Your Ad Spot

Sep 21, 2011

AMREF YATUMIA BILIONI MBILI NA USHEE KUBORESHA AFYA NA MAISHA YA WATU SERENGETI

SHIRIKA la AMREF Tanzania kupitia mradi wake wa MAJI NI UHAI limetumia sh. 2,305,580,000/= kuboresha afya na maisha ya wakazi wa wilaya ya Serengeti, mkoani Mara kwa kutengeneza miundo mbinu ya maji na kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo.
Waziri Mkuu, Mh. Mizengo Pinda, aliyeko mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ameambiwa hayo leo alipofika kijijini Nyamisingisi wilayani humu kuzindua lambo lililojengwa na AMREF kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo. Mh. Pinda pia alizindua ufugaji wa samaki kwa kupanda vifaranga 4,000 vya samaki aina ya sato.
Meneja Mipango wa AMREF Kanda ya Ziwa, Mhandisi Koronel Kema, alimwambia Waziri Mkuu kuwa lambo la Nyamisingisi, Birika la kunyweshea mifugo na Kituo cha kuchotea maji ni sehemu ya mradi wa MAJI NI UHAI unaotekelezwa katika kata za Kibanchebanche, Ringhwani, Issenye, Natta na Kyambahi kwa ufadhili wa kampuni ya ujenzi ya Ferrovial ya Hispania.
Amesema kuwa lambo hili lilijengwa na serikali mwaka 1975 lakini hadi kufikia mwaka 2007 likuwa limejaa udongo hivyo kushindwa kutumika hali iliyosababisha kukosekana kwa huduma ya josho na kibanio. Kutokana na adha kubwa ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi na mifugo yao, tulilivunja na kulijenga upya kwa sh. milioni 115 na kujenga birika la kunyweshea mifugo na kituo cha kuchotea maji kwa gharama ya sh. milioni 35.
Mhandisi Kema amesema kuwa kukamilika kwa lambo hili kumepunguza tatizo la maji kwa wakazi 3,000 wa Isenye pamoja na mifugo yao. Pia kumesaidia kupatikana kwa chanzo cha maji cha uhakika kwa ng’ombe 10,880 waliopo Nyamisingisi na vitongoji  vitatu vya kijiji cha Nyiberekera.
Hivi sasa lambo linapatia josho maji ya kutosha kuosha mifugo ambapo lina uwezo wa kuogesha ng’ombe 10,500 kwa siku ikiwa ni asilimia 70 ya ng’ombe wote kijijini. Hali hii imechangia kupunguza vifo vya ndama kutoka  asilimia 65  mwaka  2007 hadi kufikia asilimia 41 mwaka jana. Aidha josho hilo lina uwezo wa kutoa michovyo kwa mbuzi na kondoo wote 6,270.
Akielezea MAJI ni UHAI, Mhandisi Kema, amesema kuwa sh. 2,240,000,000 zilitolewa na Ferrovial wakati wananchi walihamasishwa kuchangia utekelezaji wa mradi huo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2008 ambapo walichanga sh. 65,580,000/= kwa ajili ya shughuli za maji na usafi wa mazingira.
Alisema kuwa katika kuwajengea uwezo wananchi, mradi huu umehamasisha viongozi wa vijiji na kata 646 (Wanaume 485, Wanawake 161) na wanajamii 1857(wanaume 1004 na  wanawake 853)  ili waweze kushiriki katika kupanga na kutekeleza shughuli za mradi na kuumiliki na kuwajengea jamii ufahamu na stadi za kusimamia na kufanya miundombinu ya maji na usafi wa mazingira kuwa endelevu.
Mradi umetengeneza yafuatayo na gharama yake kwenye mabano malambo mawili (sh. milioni 128), mabirika matatu ya kunyweshea mifugo (sh. milioni 45), mifumo 23 ya uvunaji wa maji ya mvua (sh.162,442,450), visima virefu  14 (sh. milioni 256),  visima vifupi 12 (sh.16,057,800), mifumo ya maji mtiririko mitatu (sh 205,120,400), uboreshaji  chemichemi mbili (sh 9,952, 544) na ujenzi wa vyoo 42 kwenye shule 16 na zahanati tano na mifumo yake ya uvunaji maji ya mvua (sh 314,325,375).
Mradi huu umeboresha afya za wananchi na kuwapunguzia  adha ya kutembea mwendo mrefu wanawake na watoto kutafuta maji kutoka km nne hadi mita 600 katika eneo la mradi.  Aidha mradi umeongeza upatikanaji wa maji katika eneo la mradi kutoka asilimia  28 mwaka 2008 mpaka asilimia  78  mwaka huu.
Takwimu kwenye vituo vya afya vilivyopo kwenye eneo la mradi zinaonyesha kuwa uhamasishaji wa matumizi  sahihi ya vyoo na usafi wa mazingira umechangia kupunguza  magonjwa yanayotokana  na ukosefu wa maji safi na salama kama kuharisha, kipindupindu, minyoo na muwasho wa ngozi   kutoka asilimia 90 mwaka 2008 mpaka asilimia  40 mwaka huu.
Mpaka sasa idadi ya kaya zisizokuwa na vyoo imepungua katika eneo la mradi  kutoka asilimia 38  mwaka 2008 mpaka asilimia 19 mwaka huu.


Kwa taarifa zaidi wasiliana na:
Agnes Kabigi, Meneja Mawasiliano, Simu: 0767 234 702

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages