Washiriki wakiwa kwenye semina hiyo |
Kauli za uchochezi, chuki, ubinafsi, ubaguzi kwa misingi ya rangi, dini, kabila, na kutengana ni baadhi ya viashiaria ambavyo kama havitatambuliwa mapema na kudhibitiwa ipasavyo vinaweza kuitumbikiza nchi yoyote ile katika hatari kubwa ya mauaji ya kimbari.
“ Ni wajibu basi wa kila serikali na kila raia kuwa macho na viashiria hivyo hasa ikizingatiwa kwamba mauaji aina hii huwa yazuki ghafla la hasha, maandalizi yake ni ya muda mrefu, yanakuwa na viongozi wake na yanapangwa”.
Hayo yameelezwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, wakati alipokuwa akifungua semina ya siku mbili kuhusu Uzuiaji wa Mauaji ya Kimbari na Wajibu wa kulinda Raia.
Semina hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uzuiaji wa Mauaji ya Kimbari ( OSAPG) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa ( UNITER) na imewahusisha wataalamu wa sheria, na haki za binadamu kutoka Balozi mbalimbali na Asasi zisizo za Kiserikali.
Balozi Manongi, amewaeleza washiriki wa semina hiyo ambayo madhumuni yake ni kujenga uwezo na uelewa kuhusu mauaji ya kimbari, vyanzo vyake, namna ya kubaini mapema viashiria hatarishi na ukusanyaji wa taarifa za awali na wajibu wa kulinda raia, kwamba mauaji ya kimbari yana mazingira yake.
Kwa hiyo, anasema Balozi mahali pa kuanzia daima ni kuielewa dhana nzima na mazingira ya mauaji ya kimbari, “tunahitaji kuelewa kwa nini yanatokea na mahusiano yake na vuguvugu za chini kwa chini, kama vile migogoro ya kugombania madaraka, rasilimali, hadhi ya uraia na haki zitokanazo na hadhi hiyo”.
“Kwa bahati nzuri, tunaweza kuzuia mauaji haya na mengine ya aina yake, kwa sababu kama nilivyosema mwanzo hayaibuki tu ghafla yana mazingira yake. Masuala kama vile misingi ya dhaifu wa kiutawala, udhaifu wa utawala wa sheria au kutokuwapo kabisa kwa utawala wa sheria ni viashiria vingine vinavyoweza kuaanda mazingira ya mauaji ya kimbari na maujaji ya halaiki”. Akasisiza Balozi.
Na kuongeza kuwa mauaji ya hayo hutanguliwa na uhalifu mwingine kama vile ubaguzi na kutengana. “Kama tunahitaji kuyashinda mauaji ya kimbari tunatakiwa kuwa macho na viashiria vya aina hii”.
Aidha akaeleza kuwa , kila serikali na kila raia anaowajibu mkubwa wa kuzibaini dalili za kuzuka kwa machafko, chuki, na uchochezi dhidi ya aina yoyote ya ubaguzi wa rangi, kabila au dini na kutoa taarifa kwa taasisi zinazohusika ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema.
“ Tunahitaji pia kuwa na misingi mizuri ya kuweza kuzigundua dalili hizo mapema hii ni pamoja na kuweza kutambua wapi au eneo gani la nchi pana dalili za kutokea kwa machafuko”.
Akasema Afrika imejifunza mengi kutokana na mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda na kwamba imejiweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na chombo cha kubaini mapema kuwapo kwa dalili za machafuko na kusisitiza pia kwamba Jumuiya ya Kimataifa nayo inayowajibu mkubwa wa kukabiliana na mauaji hayo kwa kuyadhibiti mapema kabla hayajatokea.
Aidha Balozi Manongi ameeleza pia kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) na mahakama maalumu za kimataifa kama zile za ICTR na ICTY ni vyombo ambavyo vinatakiwa kuwa sehemu ya mwisho kabisa katika mchakato mzima wa uzuaji wa mauaji ya Kimbari.
Awali akimkaribisha Balozi kufungua Semina, hiyo, Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu Bw. Adama Dieng ameeleza kwamba hakuna nchi inayoweza kujidai kwamba haitakuwa mhanga wa mauaji ya kimbari.
Akasema kwamba udhibiti wa uhalifu huo unachangamoto nyingi zikiwamo za rasimali na utashi wa kisiasa wa viongozi kukubali au kukiri mapema kwamba kuna tatizo katika nchi zao.
Akabainisha kwamba ni wajibu wa serikali kuzuia kutokea kwa mauaji ya kimbari kwa kujiwekea misingi bora ya utawala wa sheria, kuwa na mifumo ya sheria na mahakama zinazofanya kazi na kutimiza wajibu wake ipasavyo na kubwa zaidi wananchi wenye wawe na wajibu wa kuishi kama jamii moja na kuvumiliana.
Bwana Adama Dieng ambaye pia amewashi kufanya kazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda iliyoko jijini Arusha nchini Tanzania, amesema anatiwa hofu na baadhi ya mambo yanayotokea katika baadhi ya nchi hivi sasa, akitolea mfano wa Kundi la Boko Haramu , kundi ambalo limekuwa likiendesha mauaji ya raia wasiokuwa na hatia nchi Nigeria.
Akaongeza kuwa makundi ya aina hiyo ni mengine yenye silaha ni viashiria vya kutoweka kwa amani na dalili za kutokea kwa mauaji ya kimbari au halaiki, na kwamba makundi ya aina hiyo na dalili nyingine za aina yoyote ile zinatakiwa kushughulikiwa na kudhibitiwa wa nguvu zote.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269