Breaking News

Your Ad Spot

Nov 10, 2013

KENYA YAUNGA MKONO HOTUBA YA RAIS KIKWETE KUHUSU AFRIKA MASHARIKI

SERIKALI ya Kenya imewasili nchini kwa ajili ya kuiunga mkono Tanzania juu ya hatua yake ya kutangaza wazi kuwa kamwe haitojitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki licha ya baadhi ya nchi kwenda kinyume na mkataba wa jumuiya hiyo.
 
Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita katika hotuba yake aliyoitoa bungeni, alionyesha kuchukizwa na vitendo vya baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwenda kinyume na makubaliano na kusisitiza kuwa Tanzania haina mpango wa kujitoa Afrika Mashariki.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Amina Mohamed, aliyewasili nchini jana kwa ajili hiyo, alisema kuwa Serikali yake ilisoma kwa undani hotuba ya Kikwete na imefurahishwa na namna Tanzania imekuwa ikisaidia Kenya.
 
Akitetea uamuzi wa Serikali yake na baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kufanya mkutano bila kuishirikisha Tanzania, Mohamed, alisema masuala yaliyojadiliwa yalihusu pande tatu za wanachama wa jumuiya hiyo na kwamba yalikuwa ni masuala madogo ambayo hayakulenga kuingilia mikutano au makubaliano mengine ya jumuiya hiyo.
 
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari Dar es Salaam leo, alifafanua kuwa mkutano uliofanyika Mombasa, ulilenga kujadili suala la mizigo katika bandari ya Mombasa huku akisisitiza kuwa katika bandari hiyo mizigo huchukua zaidi ya siku 28 kuwasili Kampala na huchukua muda mrefu zaidi kuwasili katika nchi zisizo na bahari.
 
“Kutokana na kutofanya vizuri kwa bandari ilikuwa ni muhimu suala hilo kujadiliwa na marais hao na hakukuwa na ajenda nyingine zaidi ya hapo. Tunafahamu kuwaTanzania ni moja ya waanzilishi muhimu wa EAC,” alisema.
 
Alisema mikutano ya kamati zilizoungana kama ambayo nchi hizo tatu ziliifanya ni ya kawaida na kwamba inatarajiwa itafanyika mikutano kama hiyo zaidi huku akisisitiza kuwaTanzania nayo itakuwa  na mikutano kama hiyo.
 
“Hili ni jambo zuri, mikutano kama hii inajikita katika maeneo ambayo huenda hayajaguswa katika mikutano ya EAC. Ki ukweli jambo hili si geni na wala halihusiani kabisa na mwanachama mmoja kutengwa kwa kuwa ni muhimu kwa wanachama wote,” alifafanua.
 
Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki imekuwa ikijenga Ushirikiano ambao hadi sasa umeweka rikodi nzuri ya mafanikio huku kukiwa na michakato mingi yenye maendeleo kwa jumuiya hiyo ikiendelea kutekelezwa.
 
“Tutafanya kila tunaloweza kuhakikisha kuwa jumuiya hii inadumu ikiwa na wanachama wake watano kwa ajili ya kujiletea maendeleo kwa wananchi wote wa jumuiya hii,” alisisitiza Mohamed.
 
Aidha waziri huyo alimpongeza Rais Kikwete juu ya mchango wake na msaada kwa nchi ya Kenya huku akisisitiza kuwa nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele ikiwemo kuzungumza kwa uwazi juu ya suala la Mahakama ya Kimataifa ya  uhalifu wa Kivita (ICC) katika mkutano wa Umoja wa nchi za Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
 
“Kenya inategemea msaada wenu, bila msaada huu hatuwezi kukabiliana na suala la ICC,” alisema na kuongeza kuwa kati ya Januari na Februari mwakani, nchi wanachama wa EAC zinatarajiwa kufanya mkutano jijini Nairobi au Dar es Salaam kujadili masuala ya jumuiya hiyo.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini, Bernard Membe, alipongeza hatua hiyo ya Serikali ya Kenya kuja nchini kwa ajili ya kuuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete juu ya jumuiya ya EA.
 
Membe alisema Kenya ni ya nchi ya kwanza kuanza kuchukua hatua juu ya hotuba ya Rais Kikwete bungeni ambayo ililenga kuhakikisha kuwa jumuiya hiyo inarejea katika malengo yake ya zamani ya kuhakikisha kila mwananchama ananufaika na jumuiya hiyo.
 
Alisema katika mkutano wa jumuiya hiyo uliofanyika Aprili mwaka huu, ulijadili mambo mengi ya maendeleo ikiwemo masuala ya umeme, reli na bandari na ripoti ya masuala hayo ilitakiwa itolewe rasmi mwezi huu.
 
Alisema katika mkutano huo kulikuwa na masuala mawili ambayo Tanzania haikuyaunga mkono ambayo pia yaliungwa mkono na wanachama wengine ambayo ni masuala ya ardhi ambayo yanatakiwa yabakie chini ya mamlaka ya nchi husika.
 
“Tanzania haijawahi kupinga ajenda za jumuiya hiyo isipokuwa suala la ardhi ambalo, nchi yetu inaamini kuwa ni lazima lisiwe ajenda ya EAC, lakini masuala mengine tutafuata hatua zote zitakazokubaliwa na jumuiya hii,” alisisitiza Membe.
 
Kuhusu suala la ICC, waziri huyo alisema Tanzania imeomba rufaa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kesi inayoendelea dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ya kuongeza muda wa mwaka mmoja wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, ili kutoa muda kwa Rais huyo kushughulikia masuala ya nchi yake.
 
Alisema kwa sasa mahakama hiyo, imeahirisha kesi hiyo dhidi ya Rais Kenyatta kutoka mwezi huu hadi Februari 5, mwaka ujao.
 
Wakati akihutubia bungeni wiki iliyopita, Rais Kikwete, alisisitiza kuwa Tanzania haina mpango wa kujiondoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Alisisitiza kuwa utawala wake utahakikisha Tanzania haiwi chanzo cha jumuiya kufa na itahakikisha, yale yote yaliyokubaliwa kwenye mkataba yanatekelezwa kulingana na yalivyopangwa na si vinginevyo.
 
Jumuiya hiyo inaundwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
 
Hivi karibuni nchi tatu wanachama wa jumuiya hiyo ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania ziliunda umoja wao na kusaini makubaliano mbalimbali ikiwemo suala la Rasimu ya Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.
 
Jambo hilo, liliishangaza Tanzania na kutoa lawama kwa nchi hizo kwa madai kuwa uamuzi huo wa kujadili masuala hayo bila kushirikisha wanachama wote ni kinyume cha mkataba wa EAC

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages