Breaking News

Your Ad Spot

Aug 15, 2014

BALOZI WA TANZANIA RWANDA AWATEMBELEA AZAM FC NA KUWAAMBIA WAJITUME WAREJEE NA KOMBE DAR

Na Mahmoud Zubeiry, KIGALI 

KAIMU Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Francis Aaron Mwaipaja amewataka wachezaji wa Azam FC kujituma na kuhakikisha wanachukua Kombe la Kagame, katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, michuano inayoendelea mjini hapa.

Balozi huyo amewatembelea wachezaji hao mchana katika hoteli waliyofikia, Kigali View mjini hapa na kuwapa hamasa waweze kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.

Balozi Mwaipaja amesema kwamba amekuwa akizisikia sifa za Azam FC nchini Tanzania namna ambavyo imefuta utawala wa vigogo Simba na Yanga SC, hivyo anaamini ni timu nzuri.

 “Kitu cha msingi nataka niwaambie kwamba msifanye dharau, chezeni kwa kiwango kile kile dhidi ya kila timu muweze kushinda na kubeba Kombe, ili Tanzania ipate sifa kupitia nyinyi,”amesema.

Balozi amewasistiza wachezaji wa Azam kuelekeza nguvu na fikra zao kwenye mashindano yao ili wapeperushe vyema bendera ya Tanzania.

Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ akizungumza kwa niaba ya wachezaji amemuahidi Balozi Mwaipaja kwamba watapigana kwa nguvu zao zote kuhakikisha wanabeba Kombe.

Meneja wa Azam FC, Jemadari Said pamoja kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog nao pia wameungana na Nahodha Bocco kumuahidi Balozi taji.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara, kesho watacheza mechi yao ya mwisho ya Kundi A Kombe la Kagame dhidi ya Adama City ya Ethiopia ingawa watamkosa beki aliye katika kiwango cha juu hivi sasa, Shomary Kapombe.

Mchezaji huyo wa zamani wa AS Cannes ya Ufaransa na Simba SC ya Tanzania pia, anasumbuliwa na nyama za paja na siku ya pili leo ameshindwa kufanya mazoezi na wenzake.

Kocha Omog ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mbali na Kapombe, mshambuliaji Mhaiti pia Leonel Saint- Preux naye atakosekana- wote wakiwa wanasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Kombe liende nyumbani; Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Francis Aaron Mwaipaja (katikati) akizungumza na wachezaji wa Azam FC leo

Wachezaji wakimsikiliza Balozi leo
Kocha Joseph Omog kushoto akiteta na Msaidizi wake, Ibrahim Shikanda 





No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages