Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Agosti 20, 2014 ameanza
ziara ya Mkoa wa Morogoro kwa kuzindua Mfumo wa Huduma za Afya za Masafa – telemedicine
– katika Kituo cha Afya cha Mwaya, Wilaya ya Ulanga, ambako mtoto mchanga wa kike wa umri wa saa
chache amepewa jina la Salma, mke wa Rais Kikwete.
Rais Kikwete (Pichani), ambaye amewasili Kijiji
cha Mwaya, kwa helikopta akitokea Dar es Salaam, kuanza ziara hiyo ya siku saba
Mkoani Morogoro, ameanza kwa kuzindua Mradi Mkubwa wa Kusambaza Umeme Vijijini
Morogoro kabla ya kwenda kwenye Kituo cha Afya cha Mwaya.
Kwenye Kituo hicho cha afya, Rais
Kikwete ameambiwa na Daktari Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Godfrey Mtei kuwa
mradi umethibisha uwezo mkubwa wa kuokoa maisha ya akinamama waja wazito wakati
wa kujifungua, kutokana na wataalam kubadilisha ujuzi na utaalam kwa njia ya
mtandao wa internet na simu wakati wa
kuwazalisha akinamama.
Dkt. Mtei amesema kuwa tokea mwaka
2010 kiasi cha akinamama 13,674 wamejifungulia katika vituo vya afya vitatu vya
Mwaya, Mtimbira na Mlimba ambavyo viko katika Mfumo huo katika Mkoa wa Morogoro
na kati ya hao 1,360 wamejifungua kwa upasuaji na vimetokea vifo tisa tu katika
kipindi hicho chote.
Mfumo huo unatekelezwa kwa pamoja kati
ya Serikali ya Tanzania na Shirika Lisilokuwa la Kiserikali la World
Lung Foundation ambalo linafadhiliwa, miongoni mwa taasisi nyingine, na
Bloomberg
Philanthropies, unatekelezwa katika Mikoa ya Pwani, Morogoro na Kigoma.
Miongoni mwa mambo mengine, World
Lung Foundation linagharimia vifaa kama simu, kompyuta mpakato (laptops), moderms, linatoa mafunzo kwa watumishi wawili wawili kutoka kila
moja ya vituo vya afya ambako Mfumo huo unaendeshwa na kutoa gharama ya vituo
kuunganishwa kwenye mtandao.
Aidha, chini ya Mpango wa Kuboresha
Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto, Shirika hilo pia linajenga vyumba vya upasuaji
ikiwa ni pamoja na kutoa tiba stahiki, wadi za wazazi, uboreshaji wa mifumo ya
maji na umeme kwa kuweka jenereta na sola, kujenga nyumba za watumishi na kutoa
mafunzo mahsusi kwa watumishi wapatao 106.
Mara baada ya kuzindua Mfumo huo, Rais
Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete amemtembelea wodini mtoto wa
kike ambaye amezaliwa leo hii chini ya Mfumo huo. Mama yake mtoto huyo ameamua
kumpa mtoto huyo jina la Salma (la Mama Kikwete) mara baada ya Mama Salma
kumbeba na kumfurahia mtoto huyo.
Kwenye makao makuu ya Wilaya ya Ulanga
ya Mahenge, Rais Kikwete amezindua Hosteli ya wasichana katika Shule ya
Sekondari ya Nawenge na pia kupokea madawati 100 kwa ajili ya shule ya msingi
ya Epanko ambayo yametolewa na Kampuni ya Kibaran Resources ya Australia ambayo
inafanya maandalizi ya uchumbaji wa madini ya uno – graphite – katika wilaya
hiyo. Shule ya Sekondari ya Nawenge ina wanafunzi 475 na walimu 26. Aidha, Rais
Kikwete amezindua mradi wa maji wa mjini Mahenge ambao umegharimiwa na Serikali
kwa kiasi cha sh. milioni 433.7. Mradi huo umejengwa kutokana na ahadi ya Rais
Kikwete ya mwaka 2008 wakati alipotembelea Wilaya ya Ulanga.
Rais Kikwete pia amesimama Kijiji cha
Lupiro ambako amezindua maghala ya kuhifadhi mchele baada ya kuwa
umepukuchuliwa kutoka kwenye mpunga na kuhutubia mkutano wa hadhara ambako
wananchi wametoa kilio chao kutokana na ukosefu la soko la uhakika la mchele.
Baada ya Lupiro, Rais Kikwete ameingia
katika Wilaya ya Kilombero ambako ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la
Mto Kilombero ambalo ujenzi wake umekuwa unazungumzwa na kupangwa kutokea mwaka
wa fedha wa 1967-1968.
Rais Kikwete leo, Alhamisi, Agosti 21,
2014 anaendelea na ziara yake katika Mkoa huo wa Morogoro kwa kutembelea Wilaya
ya Morogoro.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269