Breaking News

Your Ad Spot

Mar 10, 2015

EU, UN WAFAGILIA JUHUDI ZA KUBORESHA HALI ZA WANAWAKE TANZANIA.

un2
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akitoa salamu za Umoja wa Mataifa kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro miwshoni mwa juma.

Na Modewjiblog team, Morogoro
SERIKALI ya Tanzania imepongezwa na Umoja wa mataifa kwa juhudi zake kubwa inazofanya katika kuhakikisha kuna usawa wa jinsia nchini humu.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez wakati alipopewa nafasi ya kuhutubia umati wa watu waliokusanyika kusherehekea siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa ilifanyika Morogoro.

Alisema mbele ya Rais Jakaya Kikwete kwamba kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya awamu ya nne ya kutekeleza maazimio ya kimataifa kuhusu usawa wa jinsia umeifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa yanayostahili kupigiwa mfano.

Akitoa salamu za Umoja wa Mataifa kutoka kwa Katibu Mkuu Ban Ki Moon, mratibu huyo alisema kwamba katika bara la Afrika Tanzania imefanya makubwa katika kuhakikisha usawa wa jinsia na wanawake kuwezeshwa katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kisiasa na utawala.
un6
Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Filiberto Ceriani Sebregondi akisoma risala wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.

Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya usawa kijinsia na kutolea mfano wa kuwapo kwa asilimia 36 ya wanawake Bungeni.
Aidha amesema kuanzishwa kwa mifumo inayohakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi sawa katika masuala ya uongozi, elimu na pia kupitishwa kwa sheria kali ya kukabiliana na masuala ya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake.

Aidha alisema kwamba miaka 20 iliyopita hali haikuwa sawa lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa japo yanatakiwa mengi zaidi ili kukabiliana na changamoto zilizopo sasa.

Hata hivyo ameitaka serikali kufanya  juhudi zaidi katika kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na kuhakikisha kwamba wanawake wanakuwa na sauti katika ngazi zote za utawala kuanzia katika kaya.
IMG_9262
Msanii nguli wa muziki nchini, Starah Thomas akiimba wimbo maalum katika siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.

Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa bado yapo maeneo ambapo mwanamke amekuwa akidharauliwa na pia kulazimishwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na uhuru wa mwanadamu na haki zake za msingi.

Mambo hayo ameyataja kama haki za urithi , umiliki wa ardhi, ndoa za utotoni  na ukeketaji.

Aidha kuna utata katika utekelezaji wa mifumo ya sheria inayotakiwa kumlinda mwanamke.

Mratibu huyo alisema kwamba maadhimisho hayo yanatoa nafasi ya kuchambua mafanikio, kuangalia changamoto na kutazama fursa zilizopo katika kuleta mafanikio katika juhudi za kuleta usawa wa jinsia kwa kutekeleza maazimio ya Beijing.

 Naye Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini Filiberto Ceriani Sebregondi amesema kwamba ameridhishwa sana na namna Tanzania inavyotekeleza mchakato wa kuelekea usawa wa wanawake  na maendeleo kwa wote.
IMG_9302
Msanii Peter Msechu akitoa burudani sambamba na baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari Morogoro kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.

Amesema Jumuiya hiyo imefurahishwa na nafasi  wanayopewa kusaidia Tanzania kufikia ustawi wa jamii kwa kuleta usawa kwa wanawake na wanaume.

Jumuya hiyo imesema kwamba inaamini mchango wake unasaidia kuweka hali bora zaidi kwa wanawake.

Amesema jumuiya hiyo kwa bajeti ya sasa wamechangia zaidi ya shilingi bilioni 14 katika miradi ambayo inasaidia wanawake moja kwa moja katika masuala ya wanawake katika ardhi na kilimo,ufundi stadi, fursa za ajira na kuzuia ukatili kwa wanawake.

Alisema kwamba mwaka  2014, walifanikisha  mafunzo kwa maofisa jamii 63, dawati la jinsia 150, waendesha mashtaka 200, kamati za shule 200, watu wanaojitolea 6000, pamoja na wazazi na waangalizi kutoka Tanzania na Zanzibar.

Aidha jumuiya hiyo iliwezesha wanawake 8000 wa Mtwara na Kigoma kupata mikopo, mafunzo ya biashara na kumiliki ardhi.
IMG_8516
Wanafunzi mbalimbali wa shule za sekondari mkoani Morogoro wakifurahia burudani zilizokuwa zikitolewa kwenye uwanja wa Jamuhuri yalipofanyika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani na kufikia kilele chake machi 8 mwaka huu.

Aidha wamesaidia zaidi kuendeleza mafunzo dhidi ya mila na tamaduni zinazodhalilisha wanawake mkoani mwanza na Mara.
Katika mkoa wa Morogoro wamesaidia wafumaji wa Ifakara na kuwajengea uwezo wa kuongeza kipato chao.

Aidha wamefanikisha ujenzi wa makazi katika mji Kilosa kwa wale waliovurugwa na Masika.

Katika wilaya ya Kilosa mradi huo ulitumia shilingi bilioni 13.8 kusaidia  ujenzi wa shule mbili na zahanati kupeleka umeme na maji.
IMG_8970
Kudhihirisha kuwa hata wanawake wanaweza: Mtaalamu wa Danadana Tanzania nzima hakuna, Hazala Charles Mnjeja a.k.a Ronaldo akitoa burudani kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Amesema miradi inayosaidiwa na Umoja wa Ulaya imelenga kuhakikisha kwamba wanawake na watoto wanapata nafasi ya kuchangika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aidha ameshauri watanzania kusimama kidete kuhakikisha kwamba ukatili dhidi ya wanawake na watoto unamalizwa na kuanza kutengeneza jamii inayothamini utu na usawa.

Aidha balozi huyo ametaka kuanzishwa kwa mfumo wa kushughulikia migogoro ya ardhi ili kutoa nafasi wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi unaotokana na ardhi.Alisema kuendelea kwa migogoro hiyo kunawanyima nafasi wanawake kuendelea kwa kuwa ardhi ni mtaji mkubwa kwao.
IMG_8976
IMG_9034
Sehemu ya umati wa wakazi wa Morogoro waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani wakiwemo kina baba ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.
IMG_8364
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (kushoto) na Afisa Habari wa Ubalozi wa Jumuiya ya Umoja wa ulaya Tanzania (EU), Susanne Mbise wakiwa kwenye picha ya pamoja na mtoto Miriam Edward aliyeambata na mama yake mzazi ndani ya viwanja vya Jamuhuri kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kitaifa yalifanyika mkoani Morogoro.
IMG_9355
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) akifurahi jambo wakati akiwapongeza Sister Stella Mgaya (wa pili kulia) wa Kituo cha kupambana na ukeketaji cha Masanga (TFGM) Tarime, mkoani Mara na Mkurugenzi wa Kituo hicho, Sista Germaine Baibika (wa pili kushoto) baada ya kutunikiwa tuzo ya kutambua mchango wao wa kupambana na ukeketaji kwa wasichana wilayani Tarime. Kulia ni Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Filiberto Ceriani Sebregondi.
IMG_8539
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akisalimiana kwa furaha na Mkuu wa wilaya ya Morogoro mjini, Jordan Rugimbana wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kitaifa yalifanyika mkoani Morogoro.
IMG_9337
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye picha ya pamoja na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania pamoja na viongozi wa serikali.
IMG_9330
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akiteta jambo Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya zoezi la picha ya pamoja wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani.
IMG_8415
Baadhi ya raia wa kigeni na wakazi wa Morogoro wakiingia kwenye lango kuu la uwanja wa Jamuhuri mkoani Morogoro kushiriki sherehe za siku ya wanawake duniani.
DSC_0508
Rais wa VICOBA, Tanzania Bi. Devotha Likokola  akizungumza na baadhi ya vikundi mbalimbali vya wanawake vilivyoshiriki kwenye maonyesho ya siku ya wanawake duniani mkoani Morogoro na kuwataka kujiunga na VICOBA ili waweze kupanua mitaji na wigo wa biashara zao.
IMG_8467
Afisa Utumishi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya Mashariki Esuvatie Masinga akitoa elimu ya kutambua Haki na wajibu kwa mdau wa mamlaka ya mawasiliano Tanzania kwenye banda lao wakati wa maadhimishi ya siku ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.
IMG_8367
Afisa Habari wa Jumuia ya Umoja wa ulaya Tanzania (EU), Susanne Mbise akijadiliana jambo na Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (kulia) pamoja na Stephaine Raison ambaye ni Afisa Mawasiliano wa UN Women (katikati).

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages