Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano
wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza, akizungumza na
waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, wakati alipokuwa akielezea
kuhusu kazi na majukumu ya taasisi hiyo kwa jamii, Pia udhibiti wa
bidhaa za chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba katika Vituo vya
Forodha. Kulia ni Ofisa Uelimishaji Jamii wa TFDA, James Ndege. (Picha
zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Kaimu
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),
Gaudensia Simwanza, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam
leo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Kaimu
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),
Gaudensia Simwanza, wakati wa mkutano huo, Dar es Salaam leo.
Waandishi wa habari
Napenda kwa heshima na
taadhima kutumia fursa hii kwa niaba ya Menejimenti ya TFDA na wafanyakazi wote
kwa ujumla kuwakaribisha katika mkutano huu. TFDA ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyoundwa chini ya sheria namba 1 ya Chakula, Dawa na
Vipodozi Sura 219 kwa lengo la kudhibiti ubora na usalama
wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.
Ndugu
wanahabari,
Pamoja na kazi nyingine za
kiudhibiti, TFDA imeweka taratibu na kanuni
katika kusajili, kuingiza na kutoa bidhaa hapa nchini. Leo nitazungumzia kuhusu mkakati wa wa TFDA katika udhibiti wa
bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba katika vituo vya forodha kabla ya kuruhusiwa kuingia katika soko kwa bidhaa
zinazotoka nje ya nchi au kusafirishwa nje ya nchi kwa lengo la kujiridhisha na
usalama, ubora na ufanisi wake.
Ndugu
wanahabari,
Vituo vya forodha ni vituo rasmi vya mipakani
vinavyotambulika kisheria kwa ajili ya kuruhusu uingizaji na utoaji wa bidhaa
ndani na nje ya nchi. Taasisi tofauti za usimamizi wa sheria zinakuwepo kwenye
vituo vya forordha kwa lengo la kusimamia sheria na taratibu zinazohusiana na
udhibiti wa bidhaa mbalimbali. Vituo hivyo vya forodha ni kama vile bandari,
viwanja vya ndege na bandari kavu kwa maana ya mpaka wa nchi na nchi.
TFDA imeweka
mifumo ya udhibiti wa uingizaji wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa
tiba katika vituo vya forodha ambapo kwa upande wa chakula vituo vya forodha
vinavyoruhusiwa kupitisha chakula ni
vituo 32 na kwa upande wa dawa ni vituo 10. Hii ina maana kuwa
mwingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi ni lazima aainishe kituo cha forodha
ambacho bidhaa zake zitapita wakati wa kuingiza nchini ambako kuna wakaguzi wa
bidhaa hizo. (Orodha ya vituo imeainishwa hapa chini)
Vituo vya forodha kwa ajili ya kuingiza dawa
S/N
|
Jina la Kituo cha
Forodha
|
S/N
|
Jina la Kituo cha
Forodha
|
1.
|
Namanga
|
6.
|
Kasumulu
|
2.
|
Sirari
|
7.
|
Dar es Salaam Airport
|
3.
|
Tunduma
|
8.
|
Kilimanjaro Airport
|
4.
|
Holili
|
9.
|
Dar es Salaam Seaport
|
5.
|
Horohoro
|
10.
|
Tanga Seaport
|
Vituo vya Forodha kwa ajili ya kuingiza vyakula
S/N.
|
Jina la Kituo cha Forodha
|
S/N.
|
Jina la Kituo cha Forodha
|
1.
|
Namanga
|
17.
|
Dar es Salaam Airport
|
2.
|
Sirari
|
18.
|
Kilimanjaro Airport
|
3.
|
Tunduma
|
19.
|
Kipili Seaport
|
4.
|
Holili
|
20.
|
Lindi Seaport
|
5.
|
Horohoro
|
21.
|
Mtwara Seaport
|
6.
|
Tarakea
|
22.
|
Mbamba Bay Seaport
|
7.
|
Rusumo
|
23.
|
Mwanza Seaport
|
8.
|
Mutukula/Kyaka
|
24.
|
Musoma Seaport
|
9.
|
Isaka
|
25.
|
Bagamoyo Seaport
|
10.
|
Kabanga
|
26.
|
Bukoba Seaport
|
11.
|
Kasumulu
|
27.
|
Dar es Salaam Seaport
|
12.
|
Mabamba
|
28.
|
Tanga Seaport
|
13.
|
Manyovu
|
29.
|
Itungi Seaport
|
14.
|
Mafia
|
30.
|
Kasesya Seaport
|
15.
|
Mwanza Airport
|
31.
|
Kemondo Seaport
|
Ndugu
wanahabari,
TFDA inadhibiti uingizaji wa bidhaa za chakula, dawa,
vipodozi, na vifaa tiba kwa lengo la kulinda afya za mlaji au mtumiaji dhidi ya
madhara yatokanayo na bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu. Pia,
kuhakikisha kuwa nchi yetu haifanywi kuwa jalala la bidhaa mbovu, duni na
bandia kutoka nje ya nchi na kuepusha usambazaji na uuzwaji wa dawa, chakula,
vipodozi na Vifaa tiba vyenye lebo zinazopotosha. Aidha, kwa kufanya
hivyo tunawadhibiti wafanyabiashara wasio waaminifu ambao kwa tamaa
ya pesa wanaweza kusababisha uingizaji wa bidhaa zisizo kidhi vowango vya salama
na ubora nchini.
Mfanyabiashara akitaka kuingiza
bidhaa nchini kwanza kabisa anapaswa kupata mwongozo na kanuni ili kufahamu taratibu
za usajili na uingizaji wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba nchini.
Ndugu
wanahabari,
Kwenye vituo vya forodha kuna wataalam wanaosimamia
sheria mbalimbali za nchi ambapo TFDA ni miongoni mwa taasisi zenye uwakilishi
katika vituo hivyo. TFDA imeweka
wakaguzi katika vituo vya forodha ambapo ukaguzi na usimamizi wa sheria
umeimarishwa kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama vile TRA, Jeshi la
Polisi, TBS n.k.
Wakaguzi hao wamekuwa wakifanya kazi ya kuhakikisha
bidhaa zinazorohusiwa kuingia nchini ni zenye usalama, ubora na ufanisi kwa
mujibu wa vibali vilivyoombewa. Kwa mfano, mwaka 2013/14, Mamlaka ilipokea
jumla ya maombi 11,887 ya vibali vya kuingiza nchini chakula, dawa, vipodozi na
vifaa tiba, ambapo kati ya hayo Maombi 10,341 (87%) yalitimiza vigezo na vibali
kutolewa. Maombi 1,546(13%) yalikataliwa kutokana na kutokukidhi
matakwa ya sheria na hivyo bidhaa husika kutoruhusiwa kuingizwa nchini. Vile
vile, maombi 727 ya vibali vya kusafirisha nje ya nchi chakula, dawa, vipodozi na vifaa
tiba yalipokelewa. Kati ya hayo, maombi 312 yaliidhinishwa na maombi 415 yalikuwa na hoja mbalimbali kwa sababu ya
kutokidhi matakwa ya sheria. Aidha, ukaguzi wa bidhaa katika vituo vya
forodha umeendelea kuimarika na hivyo kusaidia kudhibiti uingizaji wa bidhaa
duni na bandia nchini.
Ndugu
wanahabari,
Wakaguzi wa
TFDA katika vituo vya forodha wana jukumu la kuhakikisha kwamba kila bidhaa
inayoingizwa nchini ina kibali cha TFDA.
Kwa hivyo wakaguzi hawa hulinganisha bidhaa zilizoonyeshwa kwenye kibali
husika na bidhaa halisi iliyoingizwa.
Pia, bidhaa husika hukaguliwa kuona kama ipo katika hali nzuri ya
usalama na ubora. Aidha, maabara ndogo zinazohamishika (Mini lab Kit) hutumiwa
na wakaguzi kuchunguza sampuli za mizigo ya dawa kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini
na pia wanatumia maabara maalum (Stelite Laboratories) kuchunguza madini joto
katika chumvi kwa upande wa chakula. Pale ukaguzi na matokeo ya uchunguzi wa sampuli
za bidhaa katika kituo cha forodha unapoonyesha wasi wasi juu ya usalama na
ubora wa bidhaa husika, sampuli huchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika
Maabara kuu ya TFDA iliyoko Makao Makuu ya TFDA Dar es Salaam.
Iwapo baada ya
uchunguzi wa kimaabara, bidhaa itaonekana haikidhi viwango vilivyowekwa, amri
inatolewa kurudisha mzigo wote
ulikotoka kwa gharama ya muingizaji.
Uamuzi huu wa kurudisha
bidhaa mbovu zilikotoka unaweza kutolewa hata bila kufanya uchunguzi wa maabara
kama ubovu huo upo wazi na unaonekana kwa macho. Kwa mfano, kama mahindi yameoza au
kushambuliwa na wadudu hakuna haja ya kufanya uchunguzi wa kimaabara kabla ya
kutoa amri ya kuyarudisha yalikotoka. Pia bidhaa zisizofaa zinaweza
kuharibiwa hapa nchini kwa gharama za mwagizaji. Vilevile, bidhaa ambayo tarehe
ya mwisho ya matumizi yake (expiry date) imekaribia kumalizika haiwezi
kuruhusiwa kuingia nchini. Kwa mfano
sheria inataka bidhaa kuwa na muda wa matumizi unaozidi miezi sita kabla ya
kuruhusiwa kuingia nchini. Upungufu
mwingine ni kama bidhaa haijasajiliwa au mwingizaji hajapata kibali cha
kuingiza bidhaa husika au isiyokuwa na maelezo sahihi kwenye lebo. Pia, bidhaa zilizopigwa marufuku hazitaruhusiwa
kuingia nchini.
Ndugu
wanahabari,
Baadhi
ya changamoto tunazokabiliana nazo ni kama zifuatazo:-
· Uwepo wa
mifumo tofauti ya kiudhibiti kwa nchi za jirani;
· Bidhaa kupitia
katika vituo visivyotambulika maarufu kama “njia za panya”;
· Uingizwaji wa
bidhaa bandia na duni zilizotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu
kiasi cha kutoweza kutambulika kirahisi wakati wa ukaguzi mipakani;
· Utandawazi na
soko huria ambalo limesababisha kuongezeka kwa biashara na ushiriki wa wafanyabiashara
wengi wenye mbinu za kukwepa taratibu za udhibiti wa bidhaa;
· Uelewa mdogo
wa baadhi ya wafanyabiashara na walaji juu ya dhana nzima ya usalama na ubora
wa chakula.
Ndugu
wanahabari,
Katika
kukabiliana
na changamoto hizi, Mamlaka imeendelea kuwatumia na kuwajengea uwezo
wakaguzi wa Halmashauri,
kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kuwianisha mifumo ya udhibiti
wa
bidhaa hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC, kubuni
mbinu za kupambana na matumizi mabaya ya teknolojia na kuendelea
kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya bidhaa
zinazodhibitiwa na Mamlaka.
Ndugu
wanahabari,
Kwa kuhitimisha, naomba kwa niaba
ya TFDA nitoe shukran za dhati kwenu waandishi wa habari kwa ushirikiano ambao
mmekuwa mkiuonesha katika kutoa taarifa za kiudhibiti pale inapotokea pamoja na
kuelimisha jamii. Rai yetu kwenu ni kuendelea kutumia kalamu zenu katika
kuwaondolea hofu wananchi kuhusu usalama na ubora wa bidhaa za chakula, dawa,
vipodozi na vifaa tiba vilivyopo katika soko kutokana na mifumo thabiti
iliyowekwa na TFDA. Aidha, niwaombe msisitize
kuwabaini na kutoa taarifa kwa TFDA na Umma kuhusu vitendo vya ukiukaji sheria
na hivyo kuhatarisha maisha ya jamii.
Aidha, tunawaomba wananchi kuendelea
kutoa ushirikiano katika kuwafichua wafanyabiashara watakaovunja sheria kwa kuingiza
nchini bidhaa za chakula, dawa na vifaa tiba bila kufuata taratibu ikiwa ni
pamoja na kutumia njia za panya kwa kutoa taarifa katika ofisi za TFDA Makao
Makuu zilizipo Extenal Mabibo na ofisi za Kanda zilizopo katika mikoa ya
Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Mtwara na Dar es Salaam pamoja na Ofisi za
Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya au kituo chochote cha polisi kilicho jirani
naye.
Asanteni kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269