Wakimbizi
kutoka nchini Burundi walioko katika kambi ya Nyarugusu wakiwa
wamebeba shehena ya unga wa mahindi jana, muda mfupi baada ya kugawiwa
chakula hicho Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia chakula
(WFP), lililoweka kituo chake katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu
wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.(PICHA ZOTE NA KITENGO CHA MAWASILIANO YA
SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI).
Mkimbizi
kutoka nchini Burundi, Jacqueline Elulu (mwenye mtoto), akisubiri
kupata huduma ya afya katika kituo cha Red Cross kinachotoa huduma za
afya kwa wakimbizi walioko katika kambi ya Nyarugusu iliyoko wilayani
Kasulu mkoani Kigoma. Shirika la Red Cross ni mojawapo ya wadau
wanaoshirikiana na Serikali kutoa huduma za afya katika kambi ya
Nyarugusu.
Mkimbizi
kutoka Burundi akipata huduma ya maji katika moja ya vituo vya maji
vilivyojengwa katika Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu. Huduma za maji
safi na salama ni mojawapo ya mambo yanayotiliwa mkazo ili kulinda afya
za wakimbizi.
Idadi
ya wakimbizi kutoka Burundi wanaokimbia nchi yao na kuingia nchini
Tanzania imefikia 91,661 kwa takwimu za Jumanne, tarehe 08 Septemba,
2015. Wakimbizi hawa kwa sasa wamehifadhiwa katika Kambi ya Wakimbizi
ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Tangu
waanze kuingia mwezi Aprili mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya
nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia
wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine imekuwa ikiwapokea na kuwapa hifadhi
na huduma nyingine muhimu. Huduma hizi ni pamoja na za ulinzi, chakula,
maji, elimu na afya.
Kutokana
na kuboreshwa kwa huduma za ulinzi, hali ya ulinzi na usalama katika
kambi ya Nyarugusu na maeneo yanayoizunguka imeimarika ambapo upo
usalama wa kutosha. Kazi hii inafanywa na Polisi kwa kushirikiana na
vikundi vya ulinzi shirikishi vinavyojumuisha baadhi ya wakimbizi
wanaoishi katika kambi hii.
Kuhusu
huduma za afya, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile
Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) imeimarisha huduma hizo kwa
kuongeza idadi ya watendaji, vifaa na dawa. Kuimarishwa kwa huduma za
afya kumesaidia kudhibiti magonjwa ya mlipuko na kukabiliana na magonjwa
mengine yasiyo ya mlipuko. Upatikanaji wa maji safi na salama na
kutolewa kwa elimu ya usafi wa mazingira pia umesaidia kwa kiasi kikubwa
kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Wakati
huohuo huduma za elimu zimeimarishwa ambapo kiasi cha wanafunzi 3,889
wa elimu ya msingi na sekondari waliokuja na wazazi wao kutoka Burundi
wameandikishwa na wanaendelea na masomo.
Kabla
ya kufikia idadi hii ya sasa, wengi wa wakimbizi hawa walianza kuingia
kwa maelfu kupitia kijiji c,,ha Kagunga kilichopo mpakani na nchi ya
Burundi ambapo idadi ilianza kupungua kidogo kidogo lakini kwa siku za
hizi karibuni wakimbizi hawa wameendelea kuingilia wakiwa katika vikundi
vidogovidogo kupitia katika vijiji vingine vya mpakani na nchi ya
Burundi.
Vijiji
hivyo ni pamoja na Kilelema, Kitanga, Helushingo, Migongo,na Kigadie
vilivyopo wilayani Kasulu na Mabamba na Katanga wilayani Kibondo na
Kituo kidogo cha Uhamiaji cha Manyovu kilichopo mpakani na nchi ya
Burundi. Aidha wakimbizi wengine wamekuwa wakipitia vijiji vya
Bugarama, Kabanga na Kasange vilivyopo wilayani Ngara mkoani Kagera.
Wakimbizi
hawa ambao wamekuwa wakipokelewa katika maeneo haya wamekuwa
wakisajiliwa na hatimaye kusafirishwa hadi kambi ya wakimbizi ya
Nyarugusu ambapo kambi hiyo imekuwa ikipokea wastani wa wakimbizi mia
mbili (200) kwa siku.
Hata
hivyo kutokana na msongamano katika kambi hiyo ya Nyarugusu ambayo
awali ilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa
kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi
(UNHCR) na wadau wengine ina mpango wa kuwahamisha wakimbizi hawa kutoka
Burundi kwenda kwenye maeneo mengine.
Maeneo
hayo ambayo yameshaanza kufanyiwa maandalizi ni Mtendeli na Karago
wilayani Kakonko na Nduta wilayani Kibondo. Zoezi la kuwahamisha
wakimbizi hawa kutoka Burundi linatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi
huu.
Kuhamishwa
kwa wakimbizi hawa kutoka Burundi kutaondoa msongamano uliopo katika
Kambi ya Nyarugusu ambayo itaendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
IMETOLEWA NA:
Isaac J. Nantanga
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Nyarugusu – KIGOMA
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269