Breaking News

Your Ad Spot

Jun 2, 2016

TANZANIA YASIFIKA KWA UTAWALA WA SHERIA, ASEMA WAZIRI KAIRUKI

Waziri Angella Kairuki


NA IMMACULATE MAKILIKA- MAELEZO
Serikali ya Tanzania yasifika kwa kuwa na uongozi unaozingatiaSheria na Utawala Bora.
Hayo yamesemwa  jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki alipokuwa akifungua Mkutano wa siku mbili  wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Sheria na Utawala bora.
Lengo la mkutano huo ilikuwa ni  kujadili masuala ya Afrika katika kukuza utawala wa sheria katika utekelezaji wa agenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 na agenda ya Umoja wa Afrika ya 2063.
“Mkutano huu wa kistoria nchini Tanzania utasaidia kuleta mageuzi katika Taasisi zinazosimamia masuala ya Sera na Sheria ambayo yatachochea maendeleo mazuri katika nchi za Afrika”, alisema Waziri Kairuki.
Akiendelea kuzungumza Waziri Kairuki alisema uwepo wa Marais wastaafu kama Mhe.Benjamin Mkapa na Dkt. Jakaya Kikwete, katika mkutano huo ni ushahidi tosha wakuwepo na mafanikio ya utawala wa sheria na utawala bora nchini Tanzania.
Kwa upande wa Rais Mstaafu Mhe.Benjamin Mkapa, amesema ili Bara la Afrika liendelee Kiuchumi ni lazima watu wake wapate elimu ya uraia ili waweze kushiriki zaidi katika masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo yao pamoja na kuwepo na uongozi utakaoleta mabadiliko “transformative leadership”.
Naye, Waziri wa Haki Sudani ya Kusini Mhe. Pwanauwilla Unango amesema pamoja na kuwa Bara la Afrika lina matatizo mengi kama vita, njaa, magonjwa na ndoa za utotoni, dunia isiitazame Afrika kwa mtazamo huo pekee, bali inahitaji msaada kutoka Jumuiya za Kimataifa.
Mkutano huo wenye kauli mbiu “Kufikia agenda ya 2030 na agenda ya 2063:Utawala wa Sheria kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika”, (Achieving the 2030 agenda and agenda 2063:The rule of law as a driver of Africa’s suistainable development) , umeandaliwa na  Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria (IDLO) la nchini Italia, kwa Ushirikiano wa Serikali ya Tanzania  umehusisha wadau mbalimbali wakiwemo Mawaziri, kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mabalozi kutoka ndani na nje ya Afrika pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya kutetea Haki za Binadamu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages