Breaking News

Your Ad Spot

Nov 16, 2016

KABILA: NITAHESHIMU KATIBA, NCHI ZA ULAYA ZIACHE UCHOCHEZI

media
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, amesema kuwa taasisi za Serikali pamoja na yeye mwenyewe wataheshimu katiba ya nchi, ambapo ameahidi nchi hiyo kufanya uchaguzi ulio huru na haki.
Akihutubia bunge la kitaifa na baraza la seneti, rais Kabila amepongeza makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kutokana na mazungumzo ya kitaifa yaliyosimamiwa na mpatanishi wa umoja wa Afrika, Edem Kodjo.
Rais Kabila amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni, sasa ndio yanakuwa moyo wa nchi kuelekea mbele. "Makubaliano yaliyofikiwa ni ishara kuwa nchi ya Kongo ina uwezo wa kutatua mambo yake yenyewe bila kusaidiwa na mataifa kutoka nje," alisema rais Kabila ambaye muda mwingi alikuwa akishangiliwa na vijana walioingia bungeni.
Edem Kodjo, mpatanishi wa mzozo wa kisiasa nchini DRC.
Rais Kabila ameongeza kuwa, yeye kama rais jukumu lake ni kuhakikisha anailinda katiba ya nchi hiyo na kwa kuanzia, atahakikisha analinda makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni, ambayo yamepelea kuundwa kwa Serikali ya mseto kuelekea uchaguzi mkuu.
Aidha amewataka wanasiasa wa upinzani ambao hawakushiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa, waende ofisini kwake na kwamba atakuwa tayari kuwapokea ili na wao watie saini makubaliano ambayo amesema yatatatua sintofahamu ya kisiasa inayoshuhudiwa nchini humo.
Kiongozi huyo amewakashifu wanasiasa wa upinzani ambao amedai wanatumiwa na baadhi ya nchi za magharibi kuchochea vurugu nchini humo, ambapo ameapa kupambana nao.
"Sitakuwa tayari kuona vijana wanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kufanya vurugu, wakati wanaowatuma wanatumia mwanya huo kujificha nyuma yao, wakitaka kuona taifa la kongo likitumbukia katika machafuko," alisema rais Kabila.
Kwenye hotuba yake rais Kabila pia, ameyaonya mataifa ya magharibi yanayoingilia masuala ya ndani ya nchi yake, ambapo amesema mataifa hayo yasitarajie kuwa yatashinda ama kufanikiwa kuchochea vurugu nchini humo.
Kuhusu Mustakabali wake, rais Kabila ameendelea kusisitiza kuwa ataheshimu katiba ya nchi na taasisi zake, kauli ambayo ni wazi inaashiria kuwa hatawania tena urais wakati kipindi chake cha mpito kitakapomalizika, akimaliza uvumi uliokuwepo kuwa, huenda akatangaza nia ya kuendelea kusalia madarakani.
Rais Kabila amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni yamefikiwa na wanadamu na sio malaika na kwamba bado kuna nafasi ya huko mbeleni makubaliano hayo kufanyiwa marekebisho kwa mustakabali wa taifa hilo.
Kuhusu Usalama: Kwenye hotuba yake rais Kabila amezungumzia suala la usalama wa mashariki mwa nchi hiyo, ambapo amesema umeendelea kuimarika licha ya changamoto ambazo bado zimeendelea kushuhudiwa.
Rais Kabila amekiri kuwa suala la usalama kwenye eneo la mashariki bado ni changamoto, na kwamba kundi la FDLR na lile la wapiganaji wa kiislamu wa ADF-NALU ndio makundi yaliyosalia na ambayo yanatatiza usalama kwenye eneo hilo.
Kiongozi huyo akawahakikishia wananchi wake kuwa, jeshi la nchi hiyo pamoja na kikosi maalumu cha umoja wa Mataifa, wanaendelea na operesheni za kuwasambaratisha wapiganaji hao ambao amesema ndani ya siku chache zijazo watakuwa wamemalizwa.
Mustabali wa Uchaguzi: Hata hivyo baadhi ya raia wa DRC ambao wamezungumza na idhaa hii punde baada ya kumaliza hotuba yake, mbali na kupongeza hatua ambazo nchi yao imepiga toka kuingia madarakani kwa rais Kabila, wapo waliokosoa.
Wakosoaji wake wanadai kuwa walitarajia kuona kiongozi wao akitamka waziwazi kuwa hatawania tena kiti hicho kwenye uchaguzi ujao, suala ambalo hata hivyo rais Kabila hakusema wazi na badala yake akasisitiza kuheshimiwa kwa katiba.
Kwa upande mwingine wapo raia ambao wao wanaona kuwa hotuba ya rais Kabila ilijikita katika masuala mtambuka ya nchi hiyo, hasa uchaguzi na maridhiano ya kisiasa ambayo wamesema kupitia makubaliano yaliyotiwa saini nchi hiyo itaandaa uchaguzi ulio huru na haki.
Uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, sasa hautafanyika tena chini ya makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni na badala yake sasa, uchaguzi mwingine utaandaliwa na Serikali ya mpito itakayotangazwa hivi karibuni na unatarajiwa kufanyika mwaka 2018.
Masuala ya Kijamii na Uchumi: Rais Kabila amezungumzia maendeleo ya elimu nchini humo, ambapo amesema kuwa wakati akiingia madarakani bajeti ya elimu ilikuwa ni asilimia 6 pake yake na sasa anapoelekea kuhitimisha mihula yake, bajeti ya elimu imefikia asilimia 16.
Kuhusu miundombinu rais Kabila amekiri kuwa nchi yake bado inakabiliwa na changamoto ya miundombinu imara, akikiri kuwa usafiri pekee uliokuwa unatumiwa muda mwingi ni usafiri wa anga, lakini sasa amefanikiwa kujenga barabara imara kwenye maeneo mengi ya nchi na sasa yanafikika kwa urahisi.
Rais Kabila pia amesema huduma za Afya zimeendelea kuimarika sambamba na upatikanaji wa umeme wa uhakika nchi nzima.RFI

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages