.

MAELFU YA WANAWAKE KUANDAMANA BAADA YA KUAPISHWA DONALD TRUMP

Nov 14, 2016

Wanawake zaidi ya 66,000 wa Marekani wametangaza kuwa wapo tayari kushiriki katika maandamano makubwa yaliyopangwa kufanyika Januari 21 mwakani, siku moja baada ya kuanza kazi rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump katika Ikulu ya White House.
Maandamano hayo yaliyopewa jina la "Maandamano ya Wanawake Washington" yamewavutia watu wengi kutoka pembe mbalimbali za Marekani. Wanawake wengine 156,000 tayari wamesema wapo tayari kushiriki kwenye maandamano hayo mbali ya wale waliotangaza waziwazi kuwa watashiriki katika maandamano hayo mjini Washington.
Maandamano hayo ni sehemu ya ghasia ba maandamano yanayoshuhudiwa katika miji mbalimbali ya Marekani baada ya Donald Trump kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais wa Marekani dhidi ya  mpinzani wake Bi Hillary Clinton.
Maandamano ya wanawake wa Marekani dhidi ya Trump
Wakati huo huo Seneta Bernie Sanders wa chama cha Democrat amesema kuwa mtindo wa Electoral College yaani kura za wajumbe wa majimbo 50 ya Marekani unahitaji kuangaliwa upya baada ya kutangazwa tena mshindi mtu ambaye hakupata kura nyingi za wananchi.  
Akizungumza katika mahojiano na jarida la USA Today, Seneta huyo wa Vermony amesema kuwa ushindi aliopata rais mteule wa Marekani, Donald Trump kutoka chama cha Republican dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Democratic, Hillary Clinton unazidisha ulazima wa kufanyika mjadala muhimu kuhusu maana ya kura hizo za wajumbe wa majimbo 50 ya Marekani. Seneta Bernie Sanders amesema:" kuna udharura wa kuangaliwa mfumo mzima wa Electoral College ambao unampa madaraka ya nchi mtu ambaye hajapata kura nyingi za wananchi. Amesisitiza kuwa jambo hili linahitaji mjadala mkubwa. 
Bernie Sanders
Kura za wajumbe hao wa majimbo 50 ya Marekani ndizo zinazompa ushindi mgombea wa kiti cha urais na si kura za moja kwa moja za wananchi.
Itakumbukwa kuwa, Hillary Clinton amepata kura nyingi zaidi ya mpinzani wake, Donald Tramp katika uchaguzi wa hivi majuzi nchini Marekani  lakini Trump ametangazwa mshindi wa kiti cha rais kutokana na kupata kura nyingi zaidi za Electoral College au wajumbe wa majimbo 50 ya Marekani licha ya kupata kura chache zaidi zilizopigwa na wananchi.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช