Takwimu
zilizotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) kuhusu usalama wa waandishi wa habari zinaonyesha
kwamba kila baada ya siku tano mwandishi mmoja huuawa duniani kote.
Takwimu hizo zinakuja sambamba na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kukomesha ukatili wa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo ya UNESCO, karibu wanahabari 827 waliuawa katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita,115 kati yao wakiuawa mwaka jana pekee na
kuufanya mwaka 2015 kushikilia nafasi ya pili kwa mauaji ya waandishi
wa habari wengi katika muongo mmoja uliopita.
UNESCO
inasema nchi kadhaa zimeonyesha dhamira ya kukomesha mauaji ya waandishi
licha ya kwamba ni kesi chache zinazohusu vifo vya waandishi ambazo
zimeshughulikuwa au kupatiwa ufumbuzi.
Ripoti ya
shirika hilo kwa mwaka huu ilijikita zaidi katika usalama wa waandishi
wa habari dhidi ya mauaji katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na
imeonyesha kwamba haikuangalia madhila mengine yanayowakumba waandishi
ikiwemo utekaji nyara, kukamatwa kiholela, mateso, vitisho na
unyanyasaji.
Mataifa ya uarabuni ni hatari zaidi
Kati ya
waandishi 213 waliouawa katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015, waandishi
78 waliuawa katika mataifa ya kiarabu pekee kwa mujibu wa takwimu za
UNESCO na kuufanya ukanda huo kuwa eneo hatari kwa waandishi wa habari
kufanya kazi zao, sababu kubwa ikiwa ni vita inayoendelea katika mataifa
ya Syria, Yemen, Iraq na Libya.
Katika
kipindi hicho hicho jumla ya waandishi 58 waliualiwa Amerika ya Kusini
na ukanda wa Karibeani, 34 waliuawa Asia, barani Afrika waandishi
waliouawa ni 27 na 12 waliuawa Ulaya ya kati na mashariki.
Nusu ya
waandishi wa habari za mitandaoni waliouawa katika miaka miwili
iliyopita ni waandishi wa blogs na wale wa tovuti waliokuwa wakiripoti
juu ya vita ya Syria.
Katika
ukanda wa Afrika mashariki Sudan Kusini imeonekana kuwa na idadi kubwa
ya mauaji ya waandishi ambapo jumla ya waliouwa ilifikia tisa ikifuatiwa
na Uganda waandishi wa habari 4 huku nchi zilizosalia wakiripotiwa
kuuliwa mwandishi mmoja hadi wawili.
Waandishi
wa habari wanawake wameonekana kulengwa zaidi katika mauaji hayo
tofauti na takwimu za miaka iliyopita. Waathirika wakubwa wa mauaji hayo
ni waandishi wa habari wa ndani ukilinganisha na wale wa kigeni. Kwa
takwimu hizo UNESCO inasema uhuru wa vyombo vya habari bado umegubikwa
na giza na kwamba kasi ndogo ya kushughulikia kesi za mauaji hayo na
ongezeko la ukatili wa uhalifu dhidi ya waandishi kunaibua mijadala ya
kitaifa pamoja na kulenga kuvinyamazisha vyombo vya habari.UNESCO
inasema usalama wa waandishi wa habari utawezekana ikiwa masuala matatu
ya kuzuia, kuwalinda na kuwashitaki wanaohusika yatashughulikiwa.
Adui wa uhuru wa habari
Na katika
tathmini ya maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, waandishi wasio kuwa
na mipaka wameorodhesha jumla ya wakuu wa nchi 35 na serikali, makundi
yenye itikadi kali na idara za ujasusi ambapo kwa mara ya kwanza rais wa
Uturuki Tayyip Erdogan yupo katika orodha hiyo. Tathmini hiyo inasema
Erdogan anadhibiti kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari vya kitaifa na
kuongeza kwamba jumla ya wanahabari 130 wamefungwa huku vyombo vya
habari 140 navyo vikifungiwa nchini Uturuki. DW
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269