Hatua
yake imeibua mjadala wa ni nani atachukua nafasi yake ya Uspika. Nchini
Ujerumani inafikiriwa huenda akashindana na Angela Merkel katika
kinyang'anyiro cha Ukansela mwakani
Rais wa
bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz ametangaza rasmi kuwa ataingilia
siasa za Ujerumani mwakani. Inafikiriwa upo uwezekano kuwa huenda
atawania kiti cha ukansela. Hali itakayomweka kuwa mpinzani wa Kansela
Angela Merkel katika uchaguzi wa mwakani.
Martin
Schulz ambaye ni mwanachama wa Social Democratic SPD ametangaza nia hiyo
yake leo katika bunge la Umoja wa Ulaya, hivyo kuweka wazi wadhifa wake
wa kuwa mkuu wa bunge hilo la Umoja wa Ulaya. Swali likiwa nani
atakayechukua nafasi yake, wadadisi wa kisiasa wanasema huenda mrithi
wake akatokea kundi la wademokrasia wa kikristo EPP ambao ni wengi
katika bunge hilo. Hata hivyo kundi hilo tayari linashikilia nyadhifa za
rais wa baraza la Umoja wa Ulaya unaoshikiliwa na Donald Tusk na tume
ya urais wa jumuiya hiyo inayoshikiliwa na Jean-Claude Junker.
Akitangaza
uamuzi huo Schulz alisema: "Kumekuwa na uvumi kuhusu mustakabali wangu.
Sasa nimeshaamua sitawania uspika urais wa bunge la Umoja wa Ulaya kwa
muhula wa tatu. Mwaka ujao nitagombea kiti cha bunge la shirikisho la
Ujerumani kwa tikiti ya chama change SPD jimbo la North Rhine Vesfalia.
Haukuwa uamuzi rahisi, kwani ni heshima kuu kuwa rais wa bunge hili.
Ninashukuru kwa nafasi hiyo".
Nchini
Ujerumani, chama cha Schulz SPD, ni chama kidogo katika muungano wa
Merkel. Ikiwa Schulz mwenye umri wa miaka 60 atawania ukansela basi
atashindana na Merkel kwenye mchujo hasa ikizingatiwa Bi. Angela Merkel
alitangaza wiki jana kuwa atawania tena ukansela kwa muhula wa nne hapo
mwakani.
Haijabainika
ikiwa Schulz ambaye amehudumu kama rais wa bunge la Umoja wa Ulaya
tangu mwaka 2012, ndiye atakayekuwa mgombea mkuu wa chama chake SPD. Kwa
sasa Naibu Kansela Sigmar Gabriel ndiye anayeongoza katika chama hicho
cha SPD, lakini anakabiliwa na umaarufu wa chini kulingana na matokeo ya
kura za maoni.
Huku
chama cha SPD kikitarajiwa kumtangaza mgombea wake rasmi mwisho wa mwezi
Januari, hadi sasa hakuna uamuzi ambao umefikiwa wa ni nani atakayekuwa
mshindani wa Merkel kwenye kinyang'anyiro cha Ukansela.
Aidha
inafikiriwa huenda Schulz akawa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani,
kuchukua nafasi ya Frank Walter Steinmeier ambaye anatarajiwa kuacha
wadhifa wake mapema mwaka ujao kwani ameshateuliwa kuwania urais.DW
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269