Pichani inayoonyesha reli ya kati kwa kiwango cha Standrd Gauge iliyoanza kujengwa katika eneo la Soga mkoani Pwani.
Pichani ni mchoro wa Vituo vya Treni vitakavyokuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.
Na Frank Shija, MAELEZO
Serikali
ya Awamu ya Tano ndani ya mwaka mmoja imeanza mipango ya kuboresha
usafiri wa reli ya Kati kwa kuijenga kwa kiwango cha kimataifa yaani
Standard Gauge. Usafiri huu utaongeza fursa za kiuchumi kwani mazao ya
chakula na biashara toka mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Shinyanga,
Simiyu, Tabora na Singida kuelekea Dar es Salaam yatasafirishwa kwa
haraka.
Reli
hii itarahisisha pia usafiri wa abiria wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kati
na Magharibi. Usafiri wa treni kwa kiwango kikubwa huwa ni wa uhakika na
wa gharama nafuu. Hivyo ujenzi wa reli kwa Standard Gauge uteleta
ukombozi mkubwa wa kiuchumi kwa watu wa maeneo hayo na Taifa kwa ujumla.
Kwa
kipindi kirefu huduma ya usafiri wa treni kupitia Reli ya Kati (Central
Line Railway) imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na
maeneo ya Kanda ya ziwa na nchi za jirani zikiwemo Burundi, Rwanda,
Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Historia
inaonesha kuwa Reli ya Kati kama inavyojulikana sasa ilijengwa kati ya
mwaka 1905 hadi 1914 wakati huo ikiitwa Reli ya Tanganyika kwa kuwa
ilikuwa ikielekea Mkoani Kigoma ambako Ziwa Tanganyika linapatikana.
Kutokana
na umuhimu wake katika kukuza uchumi kupitia usafirishaji bidhaa na
huduma mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, Katika mwaka wa fedha
2016/2017 Serikali imeamua kuja na mpango kabambe wa kuifanyia maboresho
miundombinu ya reli hiyo ili iweze kwenda na wakati na kasi ya ukuaji wa uchumi.
Mpango
huo unahusisha ujenzi wa mtandao wa Reli mpya ya Kati katika Viwango
vya Kimataifa (Standard Gauge 80’) ili kuendana na kasi ya ongezeko la
mizigo.
Msemaji
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bw. William Budoya
anaeleza kuwa gharama iliyokaidiriwa kutumika kukamilisha mradi huo ni
Dola za Kimarekani Bilioni 7.6 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania
Trilioni 16.
Fedha
hizo zitatumika kugharamia ujenzi wa Kilomita 2,561 za reli kwa kiwango
cha Kimataifa . Ili kufanikisha mradi huo Serikali imepata ufadhili
kutoka Benki ya Exim ya China ambayo imekubali kutoa mkopo wenye
masharti nafuu.
Aidha,
katika kuhakikisha kuwa ujenzi huo unafanikiwa, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anakutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang Ikulu Jijini
Dar es Salaam.
Katika
mazungumzo yao Rais wa benki hiyo anamuhakikishia Rais Dkt. John
Magufuli kuwa Benki hiyo iko tayari kutoa kiasi hicho cha fedha ili
kufanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli. Pia anamuhakikishia Rais
kuwa Benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na
utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.
Akiuzungumzia
ujenzi wa Reli hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli anabainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia
kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo
Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Anasema reli hiyo mpya itakua tofauti na inayotumika sasa kutokana na uwezo wake
wa kuhimili usafirishaji wa mizigo mingi kwa kuwa inajengwa kwa kiwango
cha Kimataifa “Standard Gauge railway ” na itaanzia Dar es Salaam Mpaka
Kigoma, kupitia Tabora, Mwanza,Isaka hadi Rusumo; Kaliua -Mpanda
-Karema na Uvinza -Musongati nchini Burundi.
Katika
ufafanuzi alioutoa hivi karibuni kuhusu ujenzi wa reli hiyo wakati wa
Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma hivi karibuni,
Rais John Pombe Magufuli alisema tayari mchakato wa ujenzi wa reli hiyo
umeanza kwa kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakaye jenga Reli
hiyo.
Anasema sambamba na kazi hiyo Serikali itakarabati
matawi ya reli ya kati sehemu ya Kaliua-Mpanda ili kuboresha ufanisi
wake, kwa kutenga Sh. bilioni 5.5 za ajili ya usanifu.
Aidha,
Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano uliowasilishwa bungeni
Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango ,Dk. Philip Mpango unaeleza kuwa
Serikali imejipanga kufanya usanifu na ujenzi wa madaraja 16 kati ya 28
yaliyochakaa kati ya Dar es Salaam na Tabora.
Aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servaciaus Likwelile
akizungumza mara baada ya utiaji saini wa makubaliano wa ujenzi wa reli
hiyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu Meneja Mikopo Nafuu wa
Benki ya Exim ya China Bw. Zhu Ying anasema kuwa Dola za Kimarekani
bilioni 7.6 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 16 zitatumika kutekeleza
mradi huo.
Dkt.
Likwelile anasema hatua hiyo inawezesha kuanza kwa kazi ya upembuzi
yakinifu, usanifu na uundwaji wa timu za pamoja kuanza kuainisha
mahitaji halisi ya ujenzi wa mradi huo.
Anasema
mradi huu umekuja wakati muafaka kutokana na kwamba reli iliyopo sasa
ambayo ni ya Kiwango cha “meter gauge” haina uwezo mkubwa katika ubebaji
wake wa mizigo, hata baada ya kufanyiwa ukarabati.
Kwa
mwaka ni tani Milioni 5 za mizigo ndizo zinaweza kupitishwa na reli ya
sasa, ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo ya Kanda hii ambayo
itafikia tani Milioni 30 ifikapo mwaka 2025.
Kutokana
na uhitaji huo wa kukabiliana na uongezaji wa mizigo kwa kujenga uwezo
wa kuihudumia kwa kuwa na reli ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba
mizigo hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe
lakini pia kwa kasi ya spidi ya wastani wa kilometa 100 kwa saa hivyo
kuwezesha abiria kufika haraka zaidi sehemu wanazokwenda.
Pia wakati wa ujenzi wa reli hiyo watanzania takribani 300,000 watapata ajira kutokana na kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo.(P.T)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269