.

TRUMP NA HILLARY WATAFUTA KURA MUHIMU ZA MAJIMBO

Nov 4, 2016

Kombibild Trump Clinton (picture alliance/abaca/O. Douliery/newscom/N. Redmond)
Wakati zikiwa zimesalia siku nne tu kabla ya Wamarekani kupiga kura, Hillary Clinton na Donald Trump wamekabiliana jimboni North Carolina, kila mmoja akijaribu kunadi sera zake kwa Wamarekani
Huku wagombea hao wakitafuta umaarufu katika majimbo kadhaa muhimu ambayo yataamua matokeo ya uchaguzi wa Novemba 8, zawadi mbili kubwa  kwenye ramani ya uchaguzi huo, Florida na North Carolina, sasa yanaonekana kuwa majimbo ambayo kura kwa wagombea hao zinakaribiana sana. Hayo ni kwa mujibu wa kampuni ya uchunguzi wa maoni ya RealClearPolitics.
Mgombea wa Democratic Hillary Clinton aliwatumia vigogo akiwemo Rais Barack Obama kuimarisha kampeni zake katika mkondo wa lala salama, wakati bilionea Donald Trump akimtupa mkewe Melania ulingoni ajaribu kuirekebisha hadhi ya Mrepublican huyo
Wagombea hao walizuru maeneo tofauti ya jimbo hilo la kusini mashariki ambako wote wana asilimia 46.4 kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni.
"Najua kuna watu ambao wamekasirishwa kuhusu kilichofanyika katika kampeni hii. Watu huja na kuniambia, kuwa hawapati usingizi, kwamba matumbo yao yanawasumbua, wana maumivu ya kichwa. Nadhani kuwa hiyo ni ishara muhimu, kwa sababu huu ni uamuzi muhimu": Amesema Hillary.
Uchunguzi wa kitaifa wa CBS/New York Times ulioongoza uongozi wa Bi Clinton unapungua kwa pointi tatu, na sasa ana asilimia 44 dhidi ya asilimia 42 ya Trump, ishara kuwa mfanyabiashara huyo tajiri anapata kura za wapiga kura warepublican ambao wakati mmoja walikuwa na mashaka kuhusu kampeni zake.
Trump leo anaelekea katika majimbo ya New Hampshire, Ohio na Pennsylvania, wakati Clinton akitua Ohio na Michigan. Kampeni ya mwisho ya Clinton itakuwa jimboni Philadelphia katika mkesha wa uchaguzi ambapo ataungana na mumewe Bill Clinton, Rais Barack Obama na mkewe Michelle Obama. Melania Trump, mwanamitindo mzaliwa wa Slovenia ambaye huenda akawa mama taifa wa kwanza mzaliwa wa kigeni katika karne mbili, pia alichagua Pennsylvania kufanya kampeni yake ya kwanza pekee yake
"Mimi ni mhamiaji, na acha niwaambie, hakuna anayethamini uhuru na fursa za Marekani zaidi yangu, kama mwanamke anayejisimamia na mtu ambaye alihamia Marekani" amesema Melania. Mapenzi kwa taifa hili ni kitu kilichotuvutia wakati nilipokutana na Donald. Anapenda nchi hii, na anajua namna ya kuyatimiza mambo, sio tu kuzungumza.
Melania amesisitiza kuwa mumewe, anagombea kiti cha urais ili kuimarisha maisha ya wafanyakazi wanaoteseka na wazazi wanaoteseka kuwalea watoto wao.(P.T)

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช