Breaking News

Your Ad Spot

Feb 16, 2018

WAZIRI PINA AMUAGIZA KATIBU MKUU UVUVI, KUHARAKISHA MCHAKATO WA KUTAIFISHA MELI YA KAMPUNI YA BUAH NAGA ONE

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga  (mwenye kofia) akinyanyua samaki aina ya Jodari mara baada ya kukagua Meli ya Uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China iliyotia nanga katika bandari ya Dar eS Salaam kwa ajili ya ukaguzi. Meli hii ilipewa leseni ya kuvua samaki aina ya Jodari  na  inavua kwa kutumia mishipi. (Picha na John Mapepele).
----------
Na John Mapepele
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga  amemuagiza Katibu Mkuu Uvuvi, Dk.  Yohana Budeba kuharakisha mchakato wa kuomba kibali cha Mahakama ili kutaifisha meli ya Kampuni ya Buah Naga One ya nchini Malaysia baada ya mmiliki wa meli hiyo kukaidi amri halali ya Serikali iliyomtaka kulipa faini ya Dola 350,000 za Kimarekani ( Sh milioni 770)  ndani ya siku saba baada ya kubainika kukiuka Kanuni ya 66 ya Kanuni za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007.

Mpina  amesema, Januari 25 mwaka huu meli hiyo  ilikutwa na makosa mawili ambayo ni kukutwa na mapezi na mikia ya samaki aina ya papa 30 bila kuwepo miili yake na Kapteni wa meli hiyo Han Ming Chuan raia wa Malaysia  kukutwa  na bastola  aina ya Bereta na risasi kumi ambayo alikuwa anaimiliki kinyume cha sheria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kukagua Meli ya Uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China kwenye bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya ukaguzi ambapo aliipongeza kwa kufuata taratibu za kimataifa za ukaguzi, Waziri Mpina aliagiza vyombo vya dola kuisaka na kuichukulia hatua kali za kisheria meli ya Kampuni ya  Tai Hong No. 1 ambayo pia ilikaguliwa na kukutwa na mikia ya papa 44 bila kuwa na miili yake kinyume cha sheria za uvuvi.

Waziri Mpina alisema meli hiyo ilitoweka katika mazingira ya kutatanisha  na kuagiza  vyombo vya dola kufuatilia ili ikamatwe na hatimaye ifikishwe katika vyombo vya sheria.

“Tutahakikisha meli hii tunaikamata ili sheria ichukue mkondo wake kwa kuwa bahari ya Tanzania siyo shamba la bibi” alisisitiza Mpina.

Katika hatua nyingine Waziri Mpina amevitaka vyombo vya dola kuzisaka  hadi kuzipata meli nyingine 16 zilizopewa leseni ya kuvua katika  bahari ya Tanzania ambazo zilitoroshwa na wenye meli kwa  kushirikiana na watumishi wasio waaminifu mara baada ya kuanza kwa operesheni Jodari aliyoiunda hivi karibuni iliyojumuisha vyombo mbalimbali vya Serikali  kudhibiti uvuvi haramu.

Waziri Mpina alisema  doria hiyo pia inalenga kudhibiti utoroshaji wa samaki na mazao yake, kudhibiti  biashara haramu ya madawa ya kulevya, biashara ya binadamu, usafirishaji wa silaha na magendo, utupaji wa taka hatarishi kutoka katika meli na uhalifu wowote unaoweza kujitokeza katika maji ya nchi yetu.

Aidha Mpina alisema jumla ya meli 24 zilipewa leseni ya uvuvi wa bahari kuu ambapo hadi sasa ni meli 8 tu ndizo zilizokaguliwa huku 16 zikitoroshwa.

Waziri Mpina aliyataja baadhi ya  maeneo manne ambayo Serikali imeyafanyia maboresho katika   marekebisho ya Kanuni za uvuvi za mwaka 2009 na kuweka vifungu vipya ambavyo vitasaidia Serikali kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi kuwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa meli zote zinazokuja kuvua nchini kabla ya kuanza kuvua na baada ya kumaliza kuvua ili kubaini idadi halisi ya kiasi cha raslimali za uvuvi inayovunwa  na kutozwa kodi  halisi ili kuinua pato la taifa.

Kupakia asilimia kumi ya mabaharia wazawa katika kila meli inayokuja kuvua katika maji ya Tanzania  ili kuwajengea uwezo na na kuwapatia ajira.  

Kushusha samaki waliovuliwa bila kutarajiwa na  kukabidhi katika kwa Serikali kwa vile  ni mali ya serikali ili wauziwe wananchi kwa taratibu za kisheria ikiwa  ni pamoja na kupigwa mnada, kutoza mrabaha wa dola za kimarekani 0.4 kwa kila kilo ya samaki walengwa(targeted species) kuongeza pato la nchi.

Wakala wa meli ya  XISHIJI 37  nchini  Abdulkarim Karia Maina  kutoka kampuni ya  Scaforth Gereral Agencies ya jijini Dar es Salaam amesifu juhudi zinazofanywa na Waziri Mpina  katika kudhibiti meli zilizokuwa  zinalihujumu taifa kwa kutofuata taratibu na kusema kuwa zinapashwa kuigwa na watumishi wote katika Wizara yake.

“Mageuzi yanaofanywa na Mheshimiwa Mpina katika kudhibiti uvuvi haramu nchini yataleta mapinduzi makubwa katika sekta katika siku za hivi karibuni na kuliingizia taifa mapato makubwa” alisisitiza  Maina

 Naye Katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba alisifu  miongozo inayotolewa na Waziri Mpina  kuendeleza Sekta  ya Uvuvi na kuahidi kusimamia kikamilifu maelekezo yote ili sekta iweze kuchangia inavyositahili kwenye uchumi wa nchi yetu. 

Kwa upande wake, Bw. Wankyo Simon ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Dawati linalohusiana na Makosa ya Mazingira, amesisitiza kuwa Tanzania imejizatiti kuhakikisha kwamba Sheria zinachukua mkondo wake ili kudhibiti uhalifu wowote unaotokea katika bahari ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages