Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amesema Marekani
imepata fursa ya kipekee kutatua matatizo yanayoikabili nchi hiyo kwa
kutumia majibu ya chama cha Republican baada ya chama hicho kudhibiti
urais na bunge.
Pence aliyasema hayo katika mkutano wa vuguvugu la wahafidhina
unaofanyika mjini Oxon Hill ambao unatarajiwa kuhutubiwa na rais Donald
Trump hii leo. Pence aliutaja ushindi wa Trump katika uchaguzi wa mwaka
jana kuwa ni fursa ya maisha na hivyo kuwataka wanaharakati wa
kihafidhina kutoiharibu fursa hiyo.
Makamu wa rais Pence alisema
utawala mpya wa Trump umewapa fursa wahafidhina kuonyesha kwamba majibu
yao ndiyo sahihi kwa Marekani. Pence alisema utawala huo mpya utaiondoa
sheria ya huduma za afya na kuanzisha nyingine mbadala, akisema jinamizi
la taifa la Obamacare linakaribia kufika mwisho. Lakini aliongeza kuwa
wahafidhina wanapaswa kujiandaa na mapambano dhidi ya Wademocrat.
Mkuu wa shughuli za ikulu ya White House Reince Priebus akizungumza wakati wa mkutano wa CPAC, Maryland.
"Ndani
ya timu hii, sisi wahafidhina tunayo fursa ambayo inakuja kila baada ya
vizazi vichache, au inaweza kuja mara moja tu katika maisha. Marafiki
zangu, hii ndiyo fursa tuliyoisubiri kwa muda mrefu. Huu ndiyo wakati
wa kuonyesha kwa mara nyingine kwamba majibu yetu ndiyo majibu sahihi
kwa Marekani. Jeshi imara, nafasi zaidi za ajira, kodi kidogo, kuheshimu
katiba na maadili yalioifanya Marekani kuwa taifa kubwa na imani kubwa
katika uzuri wa watu wa Marekani," alisema Pence.
Mashaka ya wahafidhina kwa Trump
Mapema
mkuu wa shughuli za ikulu Reince Priebus aliomba uvumilivu na umoja,
akiwasihi wanaharakati kutofuja udhibiti wa Warepublican wa mabaraza
yote ya bunge pamoja na ikulu ya White House. Mshauri wa Trump Steve
Bannon aliwasilisha hoja ya kuwa mkakati wa utawala wenye msingi wake
katika kupunguza utitiri wa sheria na uzalendo wa kiuchumi katika
kujadili mikataba mipya ya kibiashara.
Utetezi wa Priebus
umetambua mashaka ya wahafidhina kuhusu rais huyo mpya, mwanachama wa
zamani wa chama cha Democratic ambaye huko nyuma alikuwa akizomewa
aktika mkutano huo. Trump ameonyesha mara kwa mara kuwa hatoi kipaumbele
kwa masuala ya kijamii ambayo wahafidhina wengi wanayapa umuhimu, na
pendekezo lake la uwekezaji mkubwa katika miundombinu limetia mashaka
dhamira yake ya kupunguza matumizi ya serikali.
Wajumbe wakielekea kwenye mkutano wa CPAC
Lakini
wakati ambapo Mrepublican akikalia kiti cha rais kwa mara ya kwanza
katika kipindi cha miaka nane, wanaharakti wengi wanasema wanahisi wana
nguvu na wako tayari kumpa nafasi. Vuguvugu la wanaharakati wa
kihafidhina lililoanzishwa muongo mmoja uliopita limekuwa kama kamati ya
ushawishi.
Rais Trump anatarajiwa kuhutubia mkutano huo
ulioingia katika siku ya tatu leo, akilenga kuimarisha ushawishi wake
katika jukwaa ambalo kw amuda mrefu limetafuta njia za kubadilisha mfumo
wa sheria za kodi za Marekani, kupunguza utitiri wa sheria za udhibiti
wa biashara na kufuta sheria ya huduma za afya ya rais wa zamani wa
Demcratic Barack Obama.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269