Breaking News

Your Ad Spot

Mar 27, 2011

DMI WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


                           Baadhi ya wafanyakazi wa DMI na mgeni rasmi
(walioko upande wa kulia) wakitazama bidhaa za nguo
kwenye maonyesho yaliyoambana na maadhimisho hayo,
kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha St. Joseph,
 Mbezi Luguluni, Dar es Salaam.
 MPANGO wa kuweka fedha kidogo kila wiki, umewezesha vikundi vya maendeleo ya wanawake vilivyoko chini ya Shirika la Mabinti wa Maria Imakulata (DMI) mjini Dar es Salaam na mkoa wa wani, kufikisha akiba ya sh. milioni 668.4,hadi sasa.

Hayo yalisemwa jana na Sista Lily wa DMI, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanywa na Wanawake wa vikundi hivyo, kwenye Viwanja vya Chou Kikuu cha St. Joseph, Mbezi Luguluni, Dar es Salaam, ambapo pia yaliambana na shughuli mbalimbali ikiwemo maonyesho ya kazi za mikono na nguo.

Alisema, mwaka 2004 kilianza kikundi kimoja, kikiwa na wanachama 15, na akiba ya sh. 200,500 na sasa kuna vikundi 350 vyenye wanawake 5575 ambapo kutokana na kuweka akiba kidogo kila wiki sasa vikundi hivyo vimefikisha kiasi cha sh. 666,465,000.

Sista Lily alisema mafanikio hayo yametokana na wanawake hao, kushika kwa makini mafundisho waliyokuwa wakipewa na Masista wa DMI, yenye lengo la kuleta chachu ya maendeleo ya wanawake kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Alisema, wanavikundi wote wamekuwa wakipewa semina na elimu bora ya uendeshaji na utunzaji fedha za mikopo ili ziweze kuzaa faida, kwa njia za kuzalisha mali katika sekta mbalimbali ikiwemo ufumaji, kilimo, biashara za maduka na biashara ndogo ndogo.

Sista Lily alisema, mbali na kuwafundisha stadi za biashara, pia hufunzwa namna na kutunza mazingira, afya zao na elimu ya mawasiliano.

Kuhusu malengo ya baadaye, Sista Lily alisema, sasa wanalenga kuanzisha muunganiko wa vikundi kitaifa ili kuleta chachu zaidi ya kimaendeleo na pia wana mpango wa kufanya kazi na asasi za kiraia.
Alisema katika mipango ya mwaka huu, zaidi ya wanawake 2000 hadi 3000 watanzisha miradi mbalimbali ya biashara, kuanzishwa mabwawa ya kisasa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika vijiji vitano ili kuwa na shamba la kisasa katika jamii husika.

Akizungumza katika sherehe hizo, mgeni rasmi, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya wanawake, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Judy Kizenga, aliipongeza DMI kwa ubunifu wake, wa kuleta mipango inayowalenga wanawake na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi huyo ambaye aliwakilisha Waziri wa wizara hiyo, alisema, wanawake na wananchi kwa jumla, wanazingatia mafundisho ya dini wakiwa na hali bora kuliko wakiwa masikini, hivyo Shirika la DMI limefikiria jambo la msingi kuhakikisha kwamba pamoja na kuwafundisha uumini wa dini lakini wanawake wanakuwa na hali bora kimaisha.

Maadhimosho ya Siku ya Wanawake Duniani, hufanyika Machi 8 ya kila mwaka, lakini DMI hawakuweza kufanya kutokana na kuwa katika majukumu mengine, ikiwemo kuhudhuria yale ya kitaifa yaliyofanyika Kibaha mkoa wa Pwani.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages