1.0 WAZO: Chama cha Waandishi wa Habari za Ukimwi Tanzania (AJAAT), kupitia ufadhili wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kinatangaza shindano la miezi mitatu kwa wandishi wa habari ya kuandika kuhusu UPATIKANAJI WA HUDUMA ZOTE MUHIMU ZA UKIMWI KWA MAKUNDI YA WATU WALIONYIMWA FURSA NA WALE WAISHIO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI ZAIDI NCHINI. Kilele cha shindano hilo litakalohusisha waandishi wa habari za magazetini, majarida, vituo vya runinga, redio, wachora vikaragosi (katuni) na mitandao ya blogu nchini, kitakuwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, – Desemba 1, 2011. Washindi wa shindano watazawadiwa fedha taslimu, ngao na vyeti vya ushiriki.
2.0 TAARIFA YA MSINGI: Programu shirikishi ya Umoja wa Mataifa kuhusu virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI (UNAIDS) inatafsiri upatikanaji huduma kwa wote kuwa ni dhamira ya dunia katika kupanua upatikanaji wa matibabu, kinga, matunzo na misaada kwa waathirika wa Ukimwi. Inahusisha jamii ambapo kila mtu anaweza kupata taarifa sahihi kuhusu UKIMWI na huduma za matunzo ya kiafya.
Lakini je, kila mtu katika yamii zetu wanapata huduma za kiafya? Kila mtu anapata elimu kuhusu UKIMWI kupitia vyombo vya habari na hivyo kumwezesha kufanya uamuzi mzuri kuhusu afya zao? Bahati mbaya majibu kwa aina hii ya maswali ni hapana. Pamoja na uwepo wa huduma nyingi za afya, siyo kila mtu katika jamii yetu ana uwezo sawa wa kupata huduma hii hata kama angehitaji na kuipata.
Nchini Tanzania, kwa mfano, makundi kama ya wanaouza miili (changudoa), wanaoishi na virusi vya ukimwi, walemavu, wanaojidunga dawa za kulevya, ombaomba , wafungwa na mashoga wanahisi kunyanyapaliwa na kubaguliwa kila siku kutokana na hisia hasi dhidi ya watu wa jamii hiyo. Hali inaweza kuwa mbaya zaidi na unyanyapaa unaohusisha Ukimwi hasa kwa wanaoishi na VVU na UKIMWI na kufanya kuwa ngumu zaidi kwa watu wa makundi hayo kupata haki za msingi na kupata huduma bora za kiafya.
Wakati huduma za UKIMWI nchini Tanzania na kwingineko inaongezeka katika baadhi ya vitengo, makundi ya waliomo kwenye mazingira hatarishi zaidi ya kuambukizwa VVU na UKIMWI yanazidi kupambana na vikwazo vya kiufundi, kisheria na vya kiutamaduni katika kupata huduma ya matunzo ya kiafya.
Zaidi ya hapo, kuna mambo yanayohusu usiri ambayo ni ya msingi kwa huduma ya Ukimwi katika visiwa vidogovidogo ambapo kila mtu anamfahamu mwenzake. Na hii inajitokeza katika maswali yanayoulizwa mara kwa mara na watu wanaohitaji huduma ya matunzo na matibabu, kwamba ‘Je, nikipata huduma hii kila mtu atajua shughuli yangu?’ Kwa hiyo changamoto ya kufanikisha upatikanaji huduma kwa wote haihusiani tu na upatikanaji wa huduma ya matunzo na matibabu, bali masuala kama unyanyapaa, ubaguzi na usiri.
Kwa hiyo, lengo la shindano hili ni kuwahamasisha waandishi wa habari wa magazeti na vyombo vya elektroniki kuandika makala na programu zitakazowawezesha watu wa makundi hayo kupata huduma bure na bora za UKIMWI na kuwawezesha kupata na kufurahia maisha chanya ambayo ni haki ya msingi kama Mtanzania mwingine yeyote.
Kimsingi, shindano hili halitawataka waandishi wa habari kuandika, kupiga picha, kuandika programu za redio na runinga tu kuhusu masuala ya haki kwa wote na yanavyohusishwa na janga la UKIMWI, bali litawataka waandishi kuibua mambo ya kisera na mipango ya serikali na mamlaka zake katika kushughulikia tatizo hili. Aidha, wataitaka sekta binafsi kuonyesha wanavyoweza kufanya kuueleza umma wa Watanzania ukweli kwamba upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI kwa wote hasa kwa walio katika hali hatarishi zaidi unaweza kupunguza kusambaa kwa VVU nchini.
3.0 UTANGULIZI: Takwimu na taarifa zilizopo za mpango wa sekta mtambuka wa kinga ya VVU na UKIMWI wa 2009 – 2012 (National Multisectoral HIV Prevention Strategy of 2009-2012) unaelezea kuwa kipaumbele katika hatua za kuchukua katika jitihada za kuzuia kasi ya maambukizi ya virusi ni kupanua huduma kwa makundi yaliyomo katika mazingira hatarishi zaidi.
Makundi ya wanaouza miili yao (changudoa), wanaoishi na VVU na UKIMWI, walemavu, wanaojidunga dawa za kulevya, ombaomba, wafungwa, mashoga na kadhalika, wanatengwa katika kupata huduma za VVU na UKIMWI kwa sababu mbalimbali pamoja na ukosefu wa huduma katika baadhi ya sehemu na unyanyapaa, ubaguzi na kutokuwepo na usiri.
Kwa hiyo masuala hayo yanatakiwa kushughulikiwa mara kwa mara kwa njia ya uhamasishaji na kusambaza taarifa kwa usahihi kusudi taifa lifanikishe upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI hususani kwa kundi lililo katika mazingira hatarishi.
4.0 SHINDANO LENYEWE: Nia ya shindano hili ni kuwahamasisha waandishi wa habari, wapiga picha za habari, wachoraji wa vikaragosi, waandishi wa makala, makala maalum, watayarishaji vipindi na watangazaji wa vyombo vya habari kufanya uchambuzi na utafiti wa kina na kutoa makala zenye uelewa mpana na kuonyesha uhusiano kati ya haki ya kupata huduma za VVU na UKIMWI. Waandishi pia watatakiwa kuonyesha athari za kisera na kijamii kama makundi yaliyo katika mazingira hatarishi hayatapata huduma za VVU na UKIMWI, na kushauri mwelekeo sahihi na bora zaidi unaopaswa kuchukuliwa.
5.0 MALENGO: Shindano pia litakuwa na malengo yafuatayo:
i. Kuhamasisha waandishi wa habari wa vyombo vyao kuandika kwa upana kuhusu uhusiano kati ya upatikanaji huduma za VVU na UKIMWI kwa wote wanaoishi katika mazingira hatarishi na uwezekano wa kuongezeka zaidi kwa maambukizi ya VVU kama watanyimwa huduma hizo.
ii. Kuoanisha masuala ya jinsia katika taarifa zao ili kuzuia/kupunguza maambukizi zaidi ya VVU katika jamii ya Tanzania.
iii. Kujaribu na kuthubutu kuibua vizuizi vya kisheria, kijamii na kitamaduni kwa makundi hayo kupata huduma za UKIMWI zinazokubalika kimataifa na kutafuta ufumbuzi wake.
iv. Kuziweka habari za UKIMWI katika hali ya kuvutia kwa kutumia mtindo wa uandishi wa habari unaohamasisha upatikanaji huduma za UKIMWI kwa wote nchini.
6.0 MATOKEO: Baada ya miezi mitatu ya shindano, waandishi wa habari wa vyombo vya elektoniki – redio, runinga; wapigapicha, waandishi wa makala, makala maalum na wa mtandao wa blogu watakuwa wameandika makala za kutosha kuhusu upatikanaji wa huduma za UKIMWI kwa wote na jinsi zinavyohusiana na kuongezeka kwa maambukizi ya VVU.
6.1 MATARAJIO: Kupungua kwa maambukizi ya VVU na UKIMWI katika jamii ya Kitanzania na kufikia mpango wa Tanzania bila UKIMWI inawezeka.
7.0 MWONGOZO WA MAUDHUI: Maswali yafuatayo yanaweza kuwaongoza waandishi wa habari katika juhudi zao za kutafuta mambo ya kuandika katika makala zao/programu zao/picha zao au vikaragosi vyao:
i. Je, ni namna/jinsi upatikanaji mbovu wa huduma za UKIMWI kwa wote na uliokubalika kimataifa unaoweza kuongeza maambukizi ya virusi nchini.
ii. Je, Matatizo gani yanayomkabili mtu aliye katika mazingira hatarishi katika kupata huduma za UKIMWI?
iii. Nani na kwa namna gani serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi anachangia/zinavyochangia katika upatikanaji wa huduma mbovu au bora za UKIMWI kwa wote.
iv. Je, mtu anapogundua amenyimwa huduma za UKIMWI zinazokubalika kimataifa afanye nini kuepuka kuchochea maambukizi mapya ya virusi?
v. Je, kuna njia yoyote ya kisheria inayomlinda mtu asinyimwe kupata huduma za UKIMWI na kama kuna uwezekano wa utekelezaji wa sheria hizo.
vi. Je, taifa linaweza kunufaika vipi kiuchumi na kijamii kama watu walio katika mazingira hatarishi watapata huduma zote kwa urahisi bila unyanyapaa au ubaguzi?
vii. 8.0 KUNDI LENGWA: Shindano lipo wazi kwa waandishi wote wa habari na makala maalum wa Tanzania kutoka vyombo vyote vya habari. Ni vyombo vya habari vya Kitanzania tu vinaruhusiwa kushiriki na waandishi watakaoleta kazi zao lazima wawe wnafanya kazi katika vyombo vya Tanzania.
9.0 MUDA: Shindano litaendelea kwa miezi mitatu (kuanzia Agosti 18 hadi Novemba 18, 2011).
10.0 MASHARITI NA VIGEZO: Yafuatayo ni masharti na vigezo vya ushiriki.
i. Waandishi wanaopenda kushiriki katika shindano ni lazima wawe wanaishi na kufanya kazi nchini Tanzania.
ii. Makala/habari na programu zitakazowasilishwa lazima zilenge makundi yaliyomo katika mazingira hatarishi zaidi Tanzania.
iii. Kazi zitakazowasilishwa lazima zionyeshe ubunifu na si zilizonakiliwa kutoka machapisho mengine. Ziwe zimetangazwa au kuchapishwa katika kipindi cha miezi mitatu ya shindano, yaani kutoka Agosti 18 mpaka Novemba 18, 2011.
iv. Ziwe zimechapishwa au kutangazwa kwenye magazeti, majarida, runinga au redio.
v. Zinaweza kuchapishwa au kutangazwa kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili.
vi. Kazi halisi tu zitakubaliwa.
vii. Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha itakuwa Novemba 22, 2011.
viii. Zawadi za fedha taslimu kuanzia 300,000/= hadi 700,000/= zitatolewa kwa washindi 15 wa kwanza watakaochaguliwa na jopo la majaji kutoka wadau mbalimbali Siku ya Ukimwi Duniani. Waandishi wote watakaoshiriki watapewa vyeti vya ushiriki.
11.0 UWASILISHAJI: Washiriki wanaruhusiwa kuwasilisha hadi makala/vipindi/machapisho matatu kwa ajili ya shindano na kupeleka kwa anuwani zifuatazo:
i. AJAAT Media Writing Competition-2011, Bahari Motors Building, Plot No. 43, Kameroun Street, Kijitonyama, P O Box 33237, tel. 0713 640520/0786 300219, DAR ES SALAAM-TANZANIA
ii. Ms Jovina Bujulu, MAELEZO/Information Auditorium Services Centre, Samora, Avenue, DAR ES SALAAM, TANZANIA
Your Ad Spot
Aug 23, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269