Rais wa Sudan Kusini amemuonya Riek Machar kiongozi wa waasi wa nchi hiyo na kumtaka ajiweke kando na siasa pamoja na madaraka.
Rais Salva Kiir ametoa indhari
hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Sudan Tribune na
kusisitiza kuwa, Riek Machar anapaswa kuheshimu mwenendo na anga ya
kisiasa inayotawala Sudan Kusini na aunge mkono serikali ya mpito na
mchakato wa makubaliano ya amani.
Aidha Salva Kiir amebainisha kuwa,
Machar ana haki ya kurejea Sudan Kusini akiwa kama raia wa kawaida na si
vinginevyo. Vuta nikuvute ya kuwania madaraka baina ya Salva Kiir na
Riek Machar imedumu kwa takribani miaka mitatu sasa na kuitumbukiza
Sudan Kusini katika vita vya ndani.
Baada ya makubaliano ya amani ya Agosti
mwaka jana, kulijitokeza matumaini katika duru za kisiasa ya kufikia
tamati vita na machafuko ya ndani katika nchi hiyo changa zaidi barani
Afrika. Katika makubaliano hayo, iliamuliwa kuundwe serikali ya umoja wa
kitaifa na kurejea mjini Juba Riek Machar.
Baada ya Machar kurejea katika mji mkuu Juba Aprili mwaka huu,
aliapishwa na kuwa Makamu wa Rais. Hata hivyo Julai mwaka huu kuliibuka
mapigano baina ya wanajeshi wa Rais Salva Kiir na kikosi kitiifu kwa
Riek Machar. Kushadidi mapigano hayo kulimfanya Riek Machar akiwa pamoja
na wafuasi wake takribani 750 waukimbie mji mkuu Juba na kuelekea
kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hatu ya serikali ya Kinshasa ya kutoa
muda wa masaa 48 kuondoka waasi wa Sudan Kusini katika ardhi yake
ulikuwa wenzo wa mashinikizo dhidi ya Machar na wafuasi wake. Kwa sasa
Machar yuko nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu. Vita huko Sudan
Kusini vilianza tena katika hali ambayo, Riek Machar alikuwa ametii
kikamilifu amri ya muhula wa masaa 48 aliutoa Rais Salva Kiir kwa Riek
Machar kwamba awe amerejea mjini Juba kabla ya kumalizika makataa
hayo. Sababu hasa ya kuzuka tena vita hivyo na kwamba, ni upande upi
uliokuwa na makosa bado haijafahamika. Pamoja na hayo, kiongozi wa waasi
anamtuhumu Rais Salva Kiir kwamba, alipanga njama za kumuua na kwamba,
amekuwa akichukua hatua moja baada ya nyingine kuelekea udikteta.
Wajuzi wa mambo wanaashiria uchanga wa nchi ya Sudan Kusini ambayo
ina umri wa takribani miaka mitano sasa na kubainisha kwamba, hawakuwa
wakitaraji kabisa kwamba, nchi hiyo ingekumbwa na mchafukoge na vita
miaka mitano tu baada ya kujitangazia uhuru na kujitenga na Sudan mnamo
Julai 11 mwaka 2011.
Licha ya hayo yote, wachambuzi wa mambo
wanaamini kuwa, kukiuka ahadi na mkataba wa amani Salva Kiir na Riek
Machar ni jambo linalobainisha uchu wa madaraka walionao mahasimu hao wa
kisiasa. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, wanasiasa
hao wamethibitisha kwamba, wakiwa katika njia ya kufikia malengo yao
wako tayari kuzitoa kafara roho za watu wasio na hatia wa Sudan Kusini.
Katika tahadhari yake ya hivi karibuni, Rais Salva Kiir ameeleza azma ya
serikali ya Juba ya kuhitimisha machafuko na kurejesha amani na
uthabiti katika nchi hiyo. Kwa upande wake, Riek Machar amemtaka Katibu
Mkuu mtarajiwa wa Umoja wa Mataifa António Guterres aisaidie nchi yake
ambayo imenasa katika kinamasi cha vita vya ndani.
Wakati huo huo Festus Mogae, Rais wa zamani wa Botswana na msimamizi
wa mwenendo wa amani wa Sudan Kusini amebainisha kwamba, hali ya usalama
inayotawala katika nchi hiyo si ya kuvumilika. Endapo Riek Machar
atalifanyia kazi onyo la Rais Salva Kiir na kujiweka kando na ulingo wa
siasa, basi inawezekana kusema kuwa, atakuwa amejitolea pakubwa kwa
ajili ya kuwaokoa wananchi wa Sudan Kusini na vita pamoja na ukosefu wa
amani na usalama.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269