Breaking News

Your Ad Spot

Oct 18, 2016

RAIS DK. MAGUFULI AOMBOLEZA WALIOKUFA KATIKA AJALI YA BASI LA BARCELONA MKOANI LINDI JANA

Rais Dk. Magufuli
DAR ES SALAAM
Rais Dk. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi, kufuatia vifo vya watu 11 katika ajali ya basi la Barcelona, jana Oktoba 17, 2016,  katika eneo la Miteja Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.

Basi hilo lenye namba T 101 CUU lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kijiji cha Mahuta katika Wilaya ya Newala Mkoani Lindi, lilipinduka baada ya gurudumu lake la kushoto kupasuka na kusababisha vifo vya watu 10 papohapo na mwingine mmoja kufariki dunia baadaye katika hospitali ya Wilaya ya Lindi, huku watu wengine 43 wakiwa wamejeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema, katika salamu zake, Rais Magufuli amesema amepokea taarifa za vifo vya watu hao kwa mshituko na huzuni kwa kuwa kwa mara nyingine Taifa limepoteza watu wake na familia zimepoteza wapendwa wao na watu ambao ziliwapenda na kuwategemea.

"Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambia naomba unifikishie salamu nyingi za pole kwa wote waliopoteza jamaa na ndugu zao katika ajali hii, kwa hakika nimeguswa sana na vifo hivi na naungana na familia za marehemu wote katika maombolezo na sala" Taarifa hiyo imemkariri Rais Magufuli akisema.

"Dk. Magufuli amewasihi wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi na amewaombea Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina na amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili waungane na familia zao na kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa", imemalizia taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages