Watu 18 wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa katika mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji nchini Niger.
Habari zinasema kuwa, mapigano hayo ya jana yalitokea katika
kijiji kimoja mjini Bangui, kusini mwa nchi karibu na mpaka na Nigeria
baada ya mifugo ya wafugaji wa kabila la Fulani kuvamia mashamba ya
wakulima wa eneo hilo.
Oumarou Mohamane, Meya wa mji wa Bangui amethibitisha kutokea
mapigano hayo na kusema kuwa, polisi walilazimika kuingilia kati na
kuzima mapigano hayo ya wakulima na wafugaji, ambapo mbali na mauaji na
majeraha, nyumba zaidi ya 15 ziliteketezwa moto.
Mapigano kati ya wakulima na wafugaji wa kuhamahama yamekuwa
yakishuhudiwa kila uchao katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika,
kutokana na uhaba wa maji na rasilimali mbali na mizozo ya ardhi.
Mbali na mapigano kati ya wafugaji na wakulima na harakati za uasi
nchini Niger, nchi hiyo ya Kiafrika vile vile imekuwa ikikabiliwa na
mashambulizi ya makundi ya kigaidi kama Boko Haram yenye makao yake
makuu katika nchi jirani ya Nigeria.
Mapema mwezi uliopita wa Mei, Wizara ya Ulinzi ya Niger ilisema kuwa
wanajeshi wake 22 wameuawa na watu wenye silaha na kwamba kundi
lililofanya shambulizi hilo limekimbilia upande wa Mali. Haikubainika
iwapo lilikuwa kundi la kigaidi au la waasi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269