Waziri Mkuu wa Ethiopia amelifanyia
marekebisho baraza lake la mawaziri katika jaribio la kutaka kuzima
maandamano na malalamiko ya watu wa makabila ya Oromo na Amhara
wanaoituhumu serikali, inayodhibitiwa na kabila la Tigray, kwamba
inawabagua .
Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn amechukua hatua hiyo wiki tatu
baada ya kutangaza hali ya hatari nchini humo ambapo wakati huo
aliahidi kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri.
Katika mabadiliko hayo, Desalegn amewateua wanasiasa wawili kutoka
kabila la Oromo kuchukua wizara mbili muhimu. Watu wa kabila hilo
wamekuwa mstari wa mbele katika maandamano na malalamiko ya miezi kadhaa
sasa dhidi ya serikali ya Addis Ababa ambayo yamepelekea kuuawa mamia
ya watu. Waandamanaji pia wanataka kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa
ambao wanashikiliwa kwa kushiriki katika maandamano ya miezi kadhaa
ambayo hadi sasa yamesababisha karibu watu 500 wapoteza maisha huku
wapinzani wakisema idadi hiyo ni kubwa zaidi kuliko iliyotnagazwa.
Hatua ya Waziri Mkuu Desalegn ya kuwapa watu wa kabila la Oromo
nafasi mbili muhimu katika baraza la mawasiri imetajwa kuwa jibu muafaka
kwa matakwa ya Waoromo. Workneh Gebeyehu wa kabila la Oromo sasa ni
waziri wa mambo ya nje, na Negeri Lencho ni waziri wa habari.
Katika mabadiliko mapya ya baraza la mawaziri ni mawaziri tisa tu wa
baraza lililopita la mawaziri 30 waliosalia katika nafasi zao. Kati ya
walioachwa bila kuguswa ni mawaziri wa ulinzi, usalama wa mataifa na
naibu waziri mkuu katika baraza la mawaziri. Jambo hilo linaonyesha wazi
kuwa, nafasi muhimu na nyeti zingali zinashikiliwa na kabila la
wachache la Tigray.
Mawaziri wapya kutoka kabila la Oromo ni wanachama wa chama tawala
cha People’s Revolutionary Democratic Front, (PRDF) ambacho kimetawala
Ethiopia kwa muda wa miaka 25. Aidha aghalabu ya wabunge ni ni wanachama
wa chama hicho na kwa msingi huo bunge hilo limeidhinisha baraza jipya
la mawaziri bila mjadala.
Waziri Mkuu Desalegn hata hivyo amesisitiza kuwa, katika mabadiliko
aliyofanyia baraza la mawaziri, kigezo kikuu hakikuwa utiifu kwa chama
tawala bali amezingatia zaidi utaalamu wa mawaziri walioteuliwa. Pamoja
na hayo, weledi wa mambo wanaamini kuwa, hata kwa kuteuliwa mawaziri
wawili kutoka kabila la Oromo, maandamano na madai ya watu wa kabila
hilo hayatamalizika.
Ni wazi kuwa waandamanaji wa kabila la Oromo magharibi mwa Ethiopia
na wale wa kabila la Amhara kaskazini mwa nchi hiyo hawatakubali
kusitisha upinzani wao kutokana tu na mabadiliko katika baraza la
mawaziri.
Kwa muda wa miaka 25 sasa chama tawala cha PRDF ambacho wafuasi wake
wengi ni wa kabila la Tigray, kimeitawala Ethiopia pasina kuwepo
maandamano. Kwa hivyo maandamano ya miezi michache iliyopita yamewashtua
watawala wa Ethiopia ambao walidhani utawala wao hauwezi kutikisika.
Ukandamizaji wa maandamano umekuwa mbaya sana kiasi cha mashirika ya
kimatiafa ya kutetea haki za binadamu kuikosoa serikali ya Addis Ababa.
Weledi wa mambo wanasema demokrasia halisi, hasa katika nchi za
Afrika, inapaswa kujumuisha watu wa makabila yote makubwa na muhimu
katika nchi sambamba na kuwepo uhuru wa maoni na vyombo vya habari.
Inasuburiwa kuona iwapo Waamhara na Waoromo wataafiki mabadiliko
mapya katika baraza la mawaziri au wataendeleza maandamano wakitaka
mabadiliko zaidi yafanyike.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269