Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram
la Nigeria limeeleza juu ya utayarifu wake wa kuwaachia huru makumi ya
wanafunzi wa kike waliowateka nyara zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Garba Shehu, msemaji wa Rais wa Nigeria amesema kundi hilo la
kigaidi limetangaza kuwa tayari kuwaachia huru wanafunzi wengine 83
iwapo serikali itakubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo na wanamgambo
hao wa kitakfiri. Aidha msemaji wa Rais wa Nigeria amesisitiza kuwa
serikali iko tayari kufanya mazungumzo na kundi hilo la kigaidi
kuhusiana na kuachiwa huru wanafunzi hao wa kike.
Alkhamisi iliyopita, wanafunzi 21 wa Shule ya Upili ya Chibok
waliachiwa huru katika eneo la Banki, kwenye mpaka wa Nigeria na
Cameroon, katika kile kilichotajwa kuwa makubaliano maalumu baina ya
serikali ya Abuja na kundi la Boko Haram. Garba Shehu, msemaji wa Rais
wa Nigeria alithibitisha habari hiyo na kusema kuwa, Shirika la Msalaba
Mwekundu na serikali ya Uswisi ndizo zilizofanikisha kuchiliwa huru
wasichana hao.
Juhudi mbalimbali yakiwemo maandamano ya kimataifa ya amani zimekuwa
zikifanyika kwa ajili ya kushinikiza kuachiwa huru wasichana wote
waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram.
Ikumbukwe kuwa, tarehe 14 Aprili 2014, kundi hilo la kigaidi
liliwateka nyara wanafunzi 276 wa kike katika eneo la Chibok, wakati
wasichana hao walipokuwa wanafanya mtihani. Wasichana 57 walifanikiwa
kutoroka mara baada ya kutekwa nyara na genge hilo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269