Hali ya taharuki imetanda katika miji kadhaa
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hususan mji mkuu Kinshasa, huku
wafanyakazi wa sekta mbalimbali wakisusia kazi kufuatia wito wa
wapinzani wanaopinga makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa jana Jumanne.
Ofisi nyingi na majengo ya kibiashara yamefungwa mchana kutwa
kutokana na taharuki hiyo, huku maafisa usalama wakionekana kushika
doria katika pembe mbalimbali za nchi. Taharuki, kimya na barabara tupu
zimetawala wilaya za Gombe na Kasa-Vubu huku shughuli za kawaida
zikionekana kuendelea katika eneo la Goma, mashariki mwa Kongo DR.
Vyama vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimewataka
wafanyakazi wote kushirikia mgomo wa kitaifa na maandamano ya nchi
nzima kuanzia leo Jumatano, kumshinikiza Rais Kabila wa nchi hiyo aachie
ngazi mwishoni mwa muhula wake wa pili unaomalizika mwishoni mwa mwaka
huu.
Jean-Marc Kabund-a-Kabund katibu wa chama kikuu cha upinzani cha
Umoja kwa Ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii nchini humo
amesema kuwa, chama hicho hakiyatambui makubaliano ya kisiasa yaliyotiwa
saini jana baina ya washiriki wa mazungumzo ya kisiasa huko Kinshasa,
mji mkuu wa nchi hiyo.
Viongozi wa chama tawala nchini Kongo DR wanadai kuwa, matatizo
yaliyopo katika mwenendo wa maandalizi, yanafanya kuwa vigumu kuitisha
uchaguzi wa rais ndani ya mwaka huu huku wapinzani wa serikali
wakimtuhumu Rais Kabila kuwa anakwamisha uchaguzi huo ili aendelee
kubaki madarakani.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269