Hitilafu na mivutano ya kisiasa kati ya nchi
za Rwanda na Burundi imepamba moto tena baada ya kuuawa raia mmoja wa
Burundi katika eneo la mpaka wa nchi hizo mbili.
Maafisa wa polisi ya Burundi wanasema kuwa askari wa Rwanda
wamempiga risasi na kumuua raia mmoja wa nchi hiyo wakati raia watatu
walipokuwa wakivuka maji ya ziwa Rweru lililoko kwenye mpaka wa nchi
hizo mbili. Raia mwingine anashikiliwa na jeshi la Rwanda. Hii ni mara
ya pili kwa raia wa Burundi kupigwa risasi na kuuawa na jeshi la Rwanda
katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Uhusiano wa nchi hizo mbili jirani umepooza na kuzorota tangu
ulipoanza mgogoro wa ndani wa Burundi Aprili mwaka jana. Kugombea na
kuchaguliwa tena Rais Pierre Nkurunziza katika uchaguzi wa mwaka jana
kumeitumbukiza Burundi katika mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao bado
unatokota. Maafisa wa serikali ya Burundi wanaituhumu Rwanda kuwa
inawasaidia na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kuiondoa madarakani
serikali ya Rais Nkurunziza. Wapinzani wa kiongozi huyo wanamtuhumu
yeye na chama tawala kuwa walifanya mapinduzi dhidi ya katiba ya nchi
hiyo na kwamba kiongozi huyo hakustahiki kugombea tena kiti cha rais
baada ya kukamilisha kipindi cha pili cha uongozi wake.
Tangu ulipozuka mgogoro wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili jirani
Burundi ilichukua uamuzi kupunguza kiwango cha biashara na Rwanda.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kwa kutilia maanani muundo wa kijamii
unaoshabihiana kati ya nchi mbili jirani za Burundi na Rwanda, kuna
wasiwasi kuwa, iwapo mgogoro wa ndani nchini Burundi utapanuka na
kushadidi zaidi yumkini ukaiathiri kwa kiwango kikubwa nchi jirani ya
Rwanda. Jamii za nchi zote mbili za Rwanda na Burundi zinaundwa na watu
wa makabila ya Hutu na Tutsi.
Mivutano kati ya makabila hayo mawili ilipandikizwa na wakoloni na
kushika kasi zaidi nchini Burundi katika kipindi cha kati ya mwaka 1993
na 2006. Wakati huo na baada ya kipindi cha miaka 25 ya utawala wa
kabila la Tutsi, Burundi ilitawaliwa na mtu kutoka kabila la Hutu baada
ya kushinda uchaguzi wa rais. Hata hivyo Melchior Ndadaye hakubakia
madarakani muda mrefu na mauaji yake yalichochea zaidi machafuko na
mapigano ya kikabila nchini humo.
Kwa vyovyote vile kuongezeka mivutano ya kisiasa baina ya Rwanda na
Burundi kunatishia amani na usalama wa eneo zima la Maziwa Makuu. Wakati
huo huo inaonekana kuwa, safari za Rais Paul Kagame wa Rwanda katika
nchi jirani za Kiafrika zinafanyika kwa shabaha ya kupata uungaji mkono
wa viongozi wa nchi hizo katika mivutano ya Kigali na nchi kama Burundi
na Ufaransa. Tarehe 10 mwezi uliopita wa Oktoba Rais Paul Kagame wa
Rwanda alitishia kukata uhusiano wa nchi yake na Ufaransa. Sababu ya
vitisho hivyo ni ripoti iliyotolewa na Kamisheni ya Kupambana na Mauaji
ya Kimbari ya Rwanda ambayo iliwatuhumu maafisa wa ngazi za juu wa jeshi
la Ufaransa kuwa walihusika katika mauaji hayo yaliyosababisha vifo vya
karibu watu milioni moja wengi wao wakiwa wa kabila la Tutsi.
Katika upande mwingine wachambuzi wa mambo wamekosoa hatua ya Burundi
ya kupunguza kiwango cha biashara kati ya nchi hiyo na Rwanda na
vilevile uamuzi wa nchi hiyo wa kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa
ya Jinai (ICC). Wachambuzi hao wanasema, hatua hiyo itaiathiri zaidi
Burundi na kuifanya itengwe zaidi kisiasa na kiuchumi. Wanasema hatua
kama hizo si za kimantiki hususan katika kipindi cha sasa ambapo Burundi
inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa, ukosefu wa usalama na
kutangatanga sehemu si ndogo ya raia hususan wa maeneo ya vijijini ambao
ndio nguvu kazi kubwa katika sekta muhimu ya kilimo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269